Nyota Spurs astaafu baada ya miaka 11 ya maumivu
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina aliyeichezea pia Sevilla, AEK Athens, Roma na River Plate alikabiliana na maumivu kwa miaka mingi na ana matumaini kuwa upasuaji wake wa hivi karibuni utampa mwanzo mpya usio na maumivu.
LONDON, ENGLAND: NYOTA aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa Tottenham Hotspur, Erik Lamela ametoa taarifa kuhusu upasuaji wake wa nyonga baada ya kulazimika kustaafu akiwa na umri wa miaka 33 kufuatia miaka 11 ya maumivu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina aliyeichezea pia Sevilla, AEK Athens, Roma na River Plate alikabiliana na maumivu kwa miaka mingi na ana matumaini kuwa upasuaji wake wa hivi karibuni utampa mwanzo mpya usio na maumivu.
Lamela ambaye mara ya mwisho kabla ya kustaa alikuwa akiichezea AEK Athens alichapisha picha zake mtandaoni akiwa hospitali, ikiwemo ile ya ya eksirei pamoja na video fupi baada ya upasuaji.
Aliandika: “Nina maumivu kidogo, lakini kwa nyonga yangu mpya natumaini kifaa hiki bandia kitakuwa mwanzo wa maisha bila maumivu. Salamu kwa wote, asanteni kwa wale wanaoendelea kuniandikia!”
Mwaka jana, Lamela alizungumzia tatizo lake la nyonga katika mahojiano na TyC Sports aliposema: “Nilistaafu kutokana na tatizo la kimwili lililokuwa likinisumbua kwa muda mrefu. Nilitaka kumaliza kazi yangu kwa njia bora zaidi nikiifurahia kadri nilivyoweza licha ya tatizo hili, ambalo lilikuwa gumu sana.”
Ameongeza kuwa tatizo hilo lilikuwa kubwa zaidi kutokana na kuchakaa kwa gegedu na ugonjwa wa osteoarthritis uliokuwa umefikia hatua ya juu.
“Miaka ya mwisho ilikuwa migumu zaidi kwa sababu nyonga yangu iliathirika zaidi na sikuweza tena kufanya mazoezi kama zamani. Ndiyo maana nililazimika kubadili namna ya mazoezi nikifanya mazoezi katikati ya wiki. Nisingeweza kucheza mechi kwa sababu nyonga yangu haikuweza kuhimili kiwango hicho cha utendaji,” amesema.
Lamela alitambulika kama nyota wa baadaye akiwa River Plate mwanzoni mwa taaluma yake kabla ya kuhamia AS Roma na baadaye kutua Spurs kwa ada ya Pauni 29 milioni.
Alikuwa kipenzi cha mashabiki kwa misimu minane akijulikana kwa mtindo wake wa kuvutia na mabao ya kipekee, ikiwemo yale ya rabona. Baada ya kuondoka Spurs, alijiunga na Sevilla kabla ya kumalizia soka lake AEK Athens, ambako alistaafu. Kwa sasa amerejea Sevilla kama sehemu ya benchi la ufundi.