Nwaneri kuvalishwa namba mpya Arsenal

Muktasari:
- Kinda huyo wa miaka 18 alikuwa moja ya wachezaji muhimu kabisa kwenye kikosi cha Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta, ambacho kipo kwenye uwezekano wa kumaliza nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imempa namba mpya ya jezi kinda wake Ethan Nwaneri kwa ajili ya msimu wa 2025/26.
Kinda huyo wa miaka 18 alikuwa moja ya wachezaji muhimu kabisa kwenye kikosi cha Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta, ambacho kipo kwenye uwezekano wa kumaliza nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo.
Msimu huu, Nwaneri amekuwa akivaa jezi yenye namba 53, akifunga mabao tisa na kuasisti mara mbili katika mechi 36 alizocheza kwenye michuano yote.
Lakini, ataonekana kwenye jezi yenye namba tofauti kabisa msimu ujao, ambayo itaachwa na mchezaji mwingine wa kikosi hicho. Nwaneri atavaa jezi namba 22 msimu huu, iliyokuwa ikivaliwa na kipa David Raya, ambaye baada ya kuwa chaguo la kwanza, atavaa jezi hiyo iliyoachwa wazi na kipa Aaron Ramsdale, aliyetimkia zake Southampton wakati wa dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Mabosi wa Emirates wanaamini jezi namba 22 italeta mambo mazuri kwa Nwaneri kama ilivyokuwa kwa Gael Clichy. Namba hiyo pia iliwahi kuvaliwa na wachezaji waliochemsha kama Yaya Sanogo, Denis Suarez na Pablo Mari.
Kinda mwenzake Nwaneri, Myles Lewis-Skelly yeye hatabadilisha namba yake kwa msimu ujao, ataendelea kuvaa jezi yenye namba 49 mgongoni. Nwaneri amecheza dakika 1,303 katika msimu wake wa kwanza Emirates, huku kocha Arteta akiwa na wasiwasi kumpa mechi nyingi kinda huyo.
Kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool, Arteta alisema: “Kuna nyakati mchezaji anacheza mechi nyingi na muda mwingine hachezi sana. Yeye amecheza mechi nyingi kuliko ilivyotarajiwa.”