NOMA SANA! Wanasoka maarufu waliowahi kufungwa jela

Thursday October 21 2021
jela pic

MUNICH, UJERUMANI. STAA wa Bayern Munich, Lucas Hernandez ataanza kutumikia kufungo chake cha miezi sita jela, Oktoba 28 baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka sharti la kutomsogelea mpenzi wake, mrembo Amelia Lorente.

Hernandez aliomba asifungwe, lakini sasa ameambiwa kwamba atachagua mwenyewe kwenda kwenye gereza la kutumia kifungo chake itakapofika Oktoba 28 huko Hispania.

Hata hivyo, Hernandez si mwanasoka pekee aliyewahi kufungwa jela.


Ian Wright

Straika wa zamani wa Arsenal, Ian Wright aliweka wazi kuhusu maisha yake ya gerezani kwamba yalimbadilisha sana kama binadamu. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19 tu, aliposhindwa kulipa faini ya barabarani na hivyo kupelekwa jela kwa wiki mbili katika gereza la Chelmsford mwaka 1982.

Advertisement

“Nimesema sitaki kurudi tena kwenye sehemu kama ile. Najua sasa napaswa kufanya mambo sahihi tu,” alisema Wright mwaka 2016.


Joey Barton

Barton alitumikia siku 74 gerezani kwenye kifungo chake cha miezi sita alichohukumiwa Mei 2008. Staa huyo, aliyekuwa akiitumikia Newcastle United wakati huo alikutwa na hatia ya kuanzisha vurugu kwenye jiji la Liverpool. Wiki sita baadaye, aliongezewa miezi minne baada ya kukiri kumuumiza mchezaji mwenzake wa zamani wa Manchester City, Ousmane Dabo.


Adam Johnson

Staa Adam Johnson ni mchezaji wa nyakati za karibuni kwenye Ligi Kuu England aliyefungwa jela kwa miaka mitatu. Johnson, aliyekuwa akikipiga kwenye kikosi cha Sunderland alikutwa na hatia ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti mwenye umri mdogo, wakati alipodaiwa kutoka kimapenzi na msichana wa miaka 15 mwaka 2016.

Aliondoshwa kwenye kikosi cha Sunderland na sasa haonekani kama anaweza kurudi kwenye mchezo wa soka kwa siku za karibuni.


Duncan Ferguson

Fowadi wa zamani wa Everton, Duncan Ferguson alisema kwamba nyakati zake alizokuwa akitumikia kifungo gerezani kimeharibu sana maisha yake ya soka. Ferguson alitumikia jela siku 44 katika kifungo chake cha miezi mitatu kwenye gereza la Barlinnie huko Glasgow, Scotland mwaka 1995 baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga kichwa beki wa Raith Rovers, Jock McStay. Kipindi hicho alikuwa akiichezea Rangers na tukio lilitokea ndani ya uwanja, lakini likiwa la kwanza kwa mchezaji Mwingereza kufungwa gerezani kwa shambulizi la uwanjani.


Tony Adams

Beki wa kati wa zamani wa Arsenal, Tony Adams aliwahi kufungwa jela, lakini staa huyo alisema jambo hilo halijamfundisha kitu chochote. Adams alitupwa jela baada ya kukutwa na hatia ya kuendesha gari akiwa amelewa mwaka 1990 na hivyo kukaa gerezani kwa siku 57. Alikuwa amepitisha kiwango cha ulevi mara 27 alipopata ajali.

Hata hivyo, Adams alisema: “Jela haijanifundisha chochote. Hakukuwa na elimu yoyote ya kuniambia kwanini nilipelekwa mahali pale. Niliona kama nipo hotelini tu.”


Eric Cantona

Fowadi gwiji wa Manchester United, Eric Cantona alitupwa jela kwa kifungo cha wiki mbili baada ya kufanya tukio lililobaki kuwa la kumbukumbu ya kudumu kwenye historia ya Ligi Kuu England. Baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya ugenini dhidi ya Crystal Palace, Cantona alimaliza hasira zake kwa shabiki wa timu pinzani baada ya kumkimbilia na kumrukia daruga la staili ya kung-fu.

Hata hivyo, Cantona alitumikia jela kwa saa tatu tu baada ya kutolewa kwa dhamana.


Jermaine Pennant

Staa wa zamani wa Arsenal na Liverpool, Jermaine Pennant aliona madhara ya kuendesha gari akiwa amelewa baada ya kuigongesha Mercedes yake kwenye taa za barabarani mwaka 2005.

Alitupwa gerezani kwa kifungo cha miezi mitatu na ingawa alitolewa baada ya kutumikia theluthi moja tu ya dhabu hiyo, alisema jambo hilo lilimfundisha mambo makubwa katika maisha yake.

“Nadhani yeyote atakayekwenda jela, atabadilika. Imenibadilisha sana na sitaki kwenda tena kule,” alisema Pennant mwaka 2011.


Marlon King

Straika wa zamani Birmingham City na Wigan, King alipelekwa gerezani mwaka 2009 kwa kipindi cha miezi 18 baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga mwanamke kiasi cha kumvunja pua.

King alifanya tukio akiwa kwenye baa ya Soho Revue, Desemba 2008 katika usiku ambao alikuwa akisherehekea mkewe kuwa mjamzito, huku akiwa ametoka kufunga bao kwenye mechi ya mapema siku hiyo. Alifungwa tena jela kwa mara ya pili mwaka 2014 baada ya kukutwa na hatia ya uendeshaji gari wa kuhatarisha maisha.


Ronaldinho

Staa, aliyewahi kushinda tuzo maarufu kabisa ya Ballon d’Or, Ronaldinho aliwahi kutumikia kifungo cha gerezani. Mbrazili huyo alisherehekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 40 akiwa gerezani huko Paraguay. Ronaldinho aliwekwa jela kwa karibu mwezi baada ya kukutwa na hatia ya kuingia Paraguay na hati bandia ya kusafiria.

Advertisement