Njia ya Mayele kufika Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Timu za Afrika ambazo zimeshakamatia tiketi ya fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 ni Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia. Hivyo, DR Congo inaweza kuongeza idadi ya timu za Afrika kwenye fainali hizo kufikia 10 endapo itashinda mechi yake moja iliyobaki kwenye mchujo.
DR Congo ya Fiston Mayele imebakiza mechi moja tu kukamatia tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika huko Amerika Kaskazini mwakani.
Timu za Afrika ambazo zimeshakamatia tiketi ya fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 ni Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia. Hivyo, DR Congo inaweza kuongeza idadi ya timu za Afrika kwenye fainali hizo kufikia 10 endapo itashinda mechi yake moja iliyobaki kwenye mchujo.
DR Congo italazimika kucheza mechi za inter-confederation play-offs ili kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Canada, Mexico na Marekani. Mechi hizo za mchujo zitafanyika Machi 2026 Amerika Kaskazini, imeripotiwa kuwa ni Mexico.
Mchujo ulivyo
Kwenye mchujo huo wa inter-confederation, kila bara lilitapa nafasi moja ya kuingiza timu kwenye mechi za mchujo isipokuwa Ulaya (UEFA) pekee. Kuna nafasi ya ziada pia imetolewa kwa bara mwenyeji. Kutokana na Canada, Mexico na Marekani kuwa wenyeji wa fainali hizo, hivyo CONCACAF itakuwa na nafasi mbili kwenye mchujo, wakati AFC, CAF, CONMEBOL na OFC zenyewe zina nafasi moja. Mechi za mchujo zitafanyika Machi, ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kuanza kwa fainali zenyewe za Kombe la Dunia. Kwa maana hiyo, mchujo wa inter-confederation utahusisha timu sita, Bolivia, DR Congo, New Caledonia, Iraq, Jamaica na Suriname.
Timu hizo sita zitapangwa kulingana na viwango vyao vya ubora kwenye chati za Fifa, ambapo timu mbili za juu zitakwenda moja kwa moja kwenye fainali za mchujo huo. Zile timu nne zilizobaki, zinachuana zenyewe kwenye hatua ya nusu fainali kupatikana mshindi wa kwenda fainali. Hiyo ina maana, timu hizo sita, zitapangwa kwenye makundi mawili, Final A na Final B.
Timu zile nne, mbili zitamenyana kwenye Final A ili kupatikana mshindi wa kwenda kucheza na timu iliyotangulia kwenye fainali ya mchujo huo kutokana na ubora wake kwenye chati za Fifa na timu nyingine mbili, zitachuana kwenye Final B ili kupata nyingine zitakazokwenda kuchuana na ile iliyotangulia kwenye fainali.
Kwenye huo mchujo wa interconfederation, ndipo mbili ndizo zitakazofuzu kwa fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 kutoka kwa timu sita zitakazochuana.
Kwa mujibu wa viwango vya Fifa, DR Congo na Iraq ndizo zitakazoingia fainali kwenye mchujo huo, huku timu zitakazochuana kwenye nusu fainali ya mchujo huo ni Jamaica itakayocheza na Bolivia, ambapo itakwenda kucheza na Iraq, wakati Suriname na New Caledonia, mshindi atakwenda kucheza na DR Congo. Mechi hizo za mchujo ni moja tu, ukifungwa unatupwa nje. Kama kutakuwa hakuna mshindi kwenye mechi ya dakika 90, zitaongezwa 30 na kama bado hakuna mshindi, itapigwa mikwaju ya penalti. Hakuna mechi ya marudiano.
Kuhusu mchujo wa Uefa
Bado kuna maajabu makubwa yanatazamiwa kutokea kwenye mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa nchi za Ulaya. Timu 16 zitachuana kusaka nafasi nne zilizobaki kwenye kuiwakilisha Uefa katika fainali hizo za Amerika Kaskazini.
Uefa itatoa timu 16 kwenda Kombe la Dunia 2026, ambapo timu 12 tayari zimeshafahamika na zimebaki timu nne, ambapo vita yake itahusisha timu 16. Mechi za mchujo zitakamilika Machi, huku droo yake ikitarajiwa kupangwa Alhamisi ya Novemba 20 huko Zurich, Uswisi. Timu 16 zilizoingia kwenye mchujo ni Slovakia, Kosovo, Denmark, Ukraine, Uturuki, Ireland, Poland, Bosnia-Herzegovina, Italia, Wales, Albania, Czech Republic, Romania, Sweden, Northern Ireland na North Macedonia.
Timu hizo zitapangwa kwa makundi manne yenye timu nne, ambapo timu za Pot 1 zitacheza na timu za Pot 4, wakati zile za Pot 2 zitapangwa kumenyana na za Pot 3. Mtindo utakaotumika ni mtoano tu, mechi moja nje, huku ikiripotiwa kutakuwa na nusu fainali mbili kabla ya kufikia fainali ya mchujo huo wa kukamatia tiketi ya kwenda Kombe la Dunia 2026.
Timu zenyewe
Pot 1: Italia, Ukraine, Uturuki, Denmark
Pot 2: Wales, Slovakia, Poland, Czech Republic
Pot 3: Kosovo, Republic of Ireland, Bosnia-Herzegovina, Albania
Pot 4: Romania, Northern Ireland, Sweden, North Macedonia