Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nini kinachofuata Usyk kuachia mikanda matatu?

USKY Pict

Muktasari:

  • Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Usyk alisema huu ni wakati mwafaka wa kuyaachia mataji hayo ili mabondia wanaofuata kwenye nafasi za juu wapate ya kuyapigania.

LONDON, ENGLAND: BINGWA wa ngumi za uzito wa juu, Oleksandr Usyk ametangaza kuachia mataji yote matatu ya dunia aliyokuwa anayamiliki ya WBC, WBA na IBF, lakini amesisitiza hajaamua kustaafu mchezo huo.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Usyk alisema huu ni wakati mwafaka wa kuyaachia mataji hayo ili mabondia wanaofuata kwenye nafasi za juu wapate ya kuyapigania.

“Hali ya hewa ni nzuri, na ni siku nzuri kusema ninayaachia mataji yote ninayoyashikilia kwa sasa,” alisema Usyk wakati akitangaza kuweka kando mataji hayo.

“Nataka mataji hayo yawe wazi ili mabondia wanaofuata wapambane kwa ajili yake. Ninaacha mataji, lakini siachi mchezo huu kwa sababu bado nina pambano langu la mwisho. Nawashukuru wote na nina heshima kubwa kwa mashirikisho yote ya ngumi. Bado kuna mengi yanakuja.”

Awali, WBC ilikuwa imemwamuru Usyk kutetea taji lake dhidi ya bingwa wa muda, Agit Kabayel, huku tarehe ya mwisho ya kufikia makubaliano ikiwa Juni 30. Badala ya kutekeleza pambano hilo la lazima, Usyk ameamua kuyaachia mataji yote matatu, hivyo kuondoa wajibu wa kutetea ubingwa dhidi ya wapinzani wa lazima.

USK 01

Hatima ya mataji hayo

WBC

Katika taji la WBC bondia Agit Kabayel anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kutangazwa bingwa kamili wa WBC. Bondia huyo mwenye rekodi ya ushindi mara 27 bila kupoteza, huku mapambano 19 akishinda kwa KO amekuwa bingwa wa muda tangu Februari 2025 baada ya kumshinda Zhilei Zhang, na baadaye alitetea taji hilo dhidi ya Damian Knyba.


WBA

Kwa upande wa WBA, Murat Gassiev tayari anamiliki taji la kawaida maarufu kama “World”, hivyo anaweza kupandishwa na kuwa bingwa kamili. Hata hivyo, WBA inaweza pia kuchagua kuandaa pambano la ubingwa wa taji lililoachwa wazi kati ya mabondia waliopo juu kwenye viwango vyao. Kwa sasa, Moses Itauma, ambaye ni namba moja kwenye viwango vya WBA anatarajiwa kupambana na Filip Hrgovic, Agosti 29, na pambano hilo linaweza kutambuliwa kama la kuwania taji hilo.

Vilevile, WBA inaweza kusubiri pambano linalotarajiwa kati ya Tyson Fury na Anthony Joshua baadaye mwaka huu na kulitangaza kuwa la kuwania ubingwa huo kutokana na hadhi na mvuto wa mabondia hao.

USK 02

IBF

Kwa upande wa IBF, Frank Sanchez, ambaye ni mshindani namba moja baada ya kumshinda Richard Torrez Jr katika pambano la mchujo mwezi Mei, anaonekana kuwa mbele zaidi kupata nafasi ya kuwania taji hilo. Nafasi ya pili kwenye viwango vya IBF ipo wazi, huku Itauma na Hrgovic wakishika nafasi ya tatu na ya nne, jambo linaloweza kufanya pambano lao kuwa la mchujo wa kumpata mpinzani wa Sanchez.


Nini kinafuata kwa Usyk?

Licha ya kuyaachia mataji hayo, Usyk ameshasema bado ana pambano la mwisho kabla ya kuhitimisha maisha yake ya ngumi. Bado haijafahamika atapambana na nani, lakini miongoni mwa majina yanayotajwa ni Rico Verhoeven, Deontay Wilder, au hata pambano la heshima dhidi ya mpinzani mwingine.