Nigeria nayo yang'oka Kombe la Dunia U20

WAWAKILISHI pekee wa Afrika waliokuwa wamesalia kwenye Fainali za Kombe la Dunia la Vijana U-20, Nigeria imeng'olewa na Korea Kusini katika mechi ya robo fainali.

Mechi hiyo iliyopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Unico Madre de Ciudades, mjini Santiago del Estero nchini Argentina, Nigeria ililala kwa bao 1-0 katika mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kuisha kwa suluhu.

Bao pekee lililoing'oa Nigeria lilifungwa dakika ya 95 kupitia Seok-Hyun Choi.

Nigeria ilikuwa timu pekee kati ya nne za Afrika iliyotinga robo fainali, kwani Senegal ilitolewa hatua ya makundi, huku Tunisia na Gambia zikitolewa 16 Bora.

Nigeria ilitinga nafasi hiyo kwa kuwanyoa wenyeji, Argentina katika hatua ya 16 Bora.

Kwa ushindi iliyopata Korea Kusini imetinga nusu fainali na sasa itacheza na Italia iliyoing'oa Colombia kwa mabao 3-1, huku nusu fainali nyingine itazikutanisha Israel iliyoitoa nishai Brazili kwa mabao 3-2 dhidi ya Uruguay iliyoitoa USA kwa mabao 2-0.

Mechi za nusu fainali zitapigwa siku za Alhamisi na Ijumaa na timu zitakazoibuka washindi zitaenda kukutana katika mechi ya fainali itakayopigwa Jumapili mara baada ya kutanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaopigwa mapema.