Ni zamu ya ‘The Blues’ Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- The Blues iliyokwenda kwenye fainali hizo zinazofanyika huko Marekani ikiwa na mzuka wa kutoka kushinda ubingwa wa Uefa Europa Conference League, itakuwa na kibarua kizito cha kuikabili Los Angeles FC, kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Jumatatu usiku.
LOS ANGELES, MAREKANI: MCHAKAMCHAKA chinja, ndicho unachoweza kusema kuhusu kasi ya michuano ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu, ambapo Chelsea itakuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na straika wao wa zamani, Olivier Giroud.
The Blues iliyokwenda kwenye fainali hizo zinazofanyika huko Marekani ikiwa na mzuka wa kutoka kushinda ubingwa wa Uefa Europa Conference League, itakuwa na kibarua kizito cha kuikabili Los Angeles FC, kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Jumatatu usiku.
Kwenye mchezo huo, Chelsea inayonolewa na Enzo Maresca itakuwa na uhakika wa kupata huduma ya mkali wake aliyerejea kwa mkopo kutokea Strasbourg, kiungo wa Kibrazili, Andrey Santos. Lakini, mechi hiyo pia inaweza kumshuhudia kwa mara ya kwanza straika, Liam Delap, akikipiga akiwa na uzi wa The Blues baada ya kunaswa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Hata hivyo, The Blues itamkosa beki Wes Fofana kwa kuwa majeruhi.
Kwa upande wa Los Angeles FC (LAFC), kwenye kikosi chao kuna wachezaji wengi wenye uzoefu wa makali ya wapinzani wao, akiwamo kipa Hugo Lloris, aliyewahi kukipiga Tottenham Hotspur na straika Giroud, ambaye baada ya kuitumikia Arsenal, alitimkia Stamford Bridge na kubeba mataji na timu hiyo, likiwamo la Europa League.
Giroud anaweza asianze kwenye mechi mechi hiyo kutokana na LAFC kuwa na upinzani mkali wa namba kwenye eneo la ushambuliaji, ambapo kocha wao anaweza kuanza na mtu hatari anayefahamika kwa jina la Denis Bouanga.
Giroud aliichezea Chelsea kuanzia Januari 2018 hadi Juni 2021, akifunga mabao 39 katika mechi 119.
Shughuli nyingine ya mikikimikiki hiyo itakuwa huko uwanjani MetLife Stadium, New Jersey katika usiku wa kuamkia Jumatatu, ambapo wakali wa Brazil, Palmeiras watakuwa na kasheshe zito la kuikabili FC Porto katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na mvuto mkali.
Mchezo mwingine wa michuano hiyo utakaofanyika alfajiri ya Jumatatu utazikutanisha Botafogo FR na Seattle Sounders FC kwenye Uwanja wa Lumen Field.
Fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu zinazofanyika huko Marekani zinatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na timu nyingi kujiandaa vizuri na kwenda na vikosi bora kabisa katika kusaka ubingwa huo utakaokwenda sambamba na zawadi ya pesa ya Pauni 100 milioni.