Ni Vlahovic, Lautaro vita ya ufungaji bora Serie A

Muktasari:

  • Lautaro amefunga mabao hayo kwenye mechi 26 alizoichezea Inter Milan msimu huu ambapo mbali ya kufunga, pia ametoa asisti mbili.

ROMA, ITALIA: VITA ya kuwania tuzo ya mfungaji bora imeendelea kupamba  moto nchini Italia ambapo hadi sasa straika wa Inter Milan, Lautaro Martinez ndiye anayeongoza akiwa na mabao 23, ingawa Dusan Vlahovic wa Juventus anaonekana kumkimbizia kimyakimya.


Lautaro amefunga mabao hayo kwenye mechi 26 alizoichezea Inter Milan msimu huu ambapo mbali ya kufunga, pia ametoa asisti mbili.


Katika orodha ya mastaa wanaogombania tuzo ya ufungaji Lautaro anashika nafasi ya tatu  kwa kupiga mashuti mengi akifanya hivyo mara 64.


Pia kwa wastani mabao hayo 23, kila moja amefunga baada ya dakika 92 ikiwa ndio wastani wa juu zaidi kuliko wa mchezaji yeyote.


Hadi sasa Lautaro anapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu Inter Milan imekuwa na kiwango bora kwa msimu huu na yeye pia amekuwa bora zaidi ukilinganisha na msimu uliopita ambapo alimaliza akiwa na mabao 21 ya Serie A.


Staa wa pili kwenye vita hiyo ni Dusan Vlahovic kutoka Juventus, ambaye amefunga mabao 15. Mabao hayo amefunga katika mechi 25 ambapo amepiga mashuti 69 akiwa ndiye mchezaji aliyepiga mashuti mengi zaidi. 


Pia Dusan ni mchezaji wa pili kwenye orodha ambaye ana wastani wa dakika chache wa kufunga kutoka bao moja hadi jingine, akifanya hivyo kila baada ya dakika 118.


Staa huyu ambaye pia ametoa asisti nne kwa sasa anaonekana kuwa ndiye mshindani sahihi wa Lautaro.