Neymar kuikosa El Clasico

Muktasari:
>>Anakabiliwa na adhabu ya kukosa mechi moja, lakini anaweza kuadhibiwa kwa kukosa mechi zaidi kutokana na kitendo chake cha kumpigia makofi mwamuzi wa akiba wakati akitoka uwanjani.
Barcelona, HISPANIA. SHIDA juu ya shida. Wakati unapokumbana na tatizo moja ambalo linakupelekesha unatazamiwa kuepuka matatizo mengine kwa ajili ya kuendelea kupambana.
Hali haipo hivyo kwa mabingwa wa Hispania, Barcelona. Kwa sasa wanatamani ardhi ipasuke.
Kuna wasiwasi mkubwa kwamba, Barcelona watamkosa staa wao wa kimataifa wa Brazil, Neymar katika pambano gumu la El Clasico ambalo lina nafasi kubwa ya kuamua bingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Hispania.
Neymar anaweza kufungiwa mechi zaidi kutokana na ugomvi aliouanzisha katika pambano la juzi usiku dhidi ya Malaga ambalo Barcelona walikubali kipigo cha mabao 2-0 wakiwa ugenini.
Staa huyo mwenye miaka 24, alipewa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 65 ya pambano hilo baada ya kumcheza rafu mbaya Diego Llorente wa Malaga, katika mchezo ambao ulitawaliwa na upinzani mkali pamoja na ugomvi wa mara kwa mara kwa wachezaji wa pande zote mbili.
Mpaka wakati Neymar akitolewa nje, Barcelona walikuwa tayari wameshapigwa bao moja lililofungwa na Sandro Ramirez na mwishowe baada ya Neymar kutolewa, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kikosi chake baada ya kupigwa bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wao, Jhony.
Mwanzoni kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda Neymar alikuwa amepokea kadi nyekundu ya moja kwa moja ambayo ingemuweka nje katika pambano la watani wa jadi, El Clasico ambalo litapigwa Aprili 23, katika dimba la ugenini Santiago Bernabeu.
Hata hivyo, ripoti ya mwamuzi, Gil Manzano ilikuwa imeonyesha kwamba staa huyo wa zamani wa Santos alikuwa amepewa kadi ya pili ya njano baada ya ile ya kwanza ambayo alizuia wazi mpira wa adhabu huku akisingizia kufunga kamba za viatu vyake mbele ya mpira.
Hata hivyo, Neymar anabakia katika matatizo na FA ya Hispania kutokana na kitendo chake cha kumpigia mwamuzi wa akiba makofi baada ya kupewa kadi nyekundu na hilo linaweza kumghaarimu zaidi kwa kuzikosa mechi dhidi ya Real Sociedad na Real Madrid.
“Baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu akiwa anakwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo aligeuka na kumpigia makofi mwamuzi wa akiba,” ilisema sehemu ya taarifa hizo kuelezea tukio la Neymar kwa mujibu wa ripoti ya mwamuzi.
Kwa mujibu wa kanuni, kadi ya pili ya njano ya Neymar ilikuwa inamfanya staa huyo akose mechi moja ijayo hivyo kuwepo katika pambano la El Clasico, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa akachukuliwa hatua na Kamati ya Nidhamu ya La Liga kutokana na kitendo chake cha kumpigia makofi mwamuzi wa akiba na endapo atafungiwa mechi moja zaidi basi atalikosa El Clasico.
Kwa kichapo cha juzi kutoka kwa Malaga, Barcelona sasa inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 69 huku Real Madrid ambayo ilitoka sare na Atletico Madrid siku hiyo ikiwa inaendelea kuongoza Ligi kwa kuwa na pointi 72 huku Barca wakiwa mechi moja zaidi.
Endapo Barcelona wangeshinda katika pambano la juzi wangelingana pointi na Madrid huku wakiongoza La Liga kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo, wababe hao wa Catalunya wana wastani mzuri zaidi.
Msimu huu Neymar ameonekana kuwa mchezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Barcelona huku mastaa wenzake kutoka katika Bara la Amerika Kusini, Lionel Messi na Luis Suarez wakionekana kupwaya tofauti na ilivyokuwa katika msimu uliopita.
Hata hivyo, Neymar atarudi uwanjani kesho katika pambano la kwanza la robo fainali la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Juventus jijini Turin, Italia kutokana na kanuni za La Liga kutoingiliana na zile za Uefa.