Neymar kufanyiwa upasuaji, daktari wa timu ya taifa kuhusika
Muktasari:
- Neymar, ambaye ni raia wa Brazil na miongoni mwa wachezaji mashuhuri zaidi duniani, alikabiliana na changamoto kubwa baada ya kuamua kucheza mechi tatu akiwa na jeraha hilo.
Baada ya kuinusuru Santos FC kutoshuka daraja katika Ligi Kuu ya Brazil, mshambuliaji Neymar Jr., anatarajiwa kufanyiwa upasuaji muhimu wa goti, jeraha ambalo amekuwa akilidhibiti kwa miezi kadhaa huku akiendelea kucheza.
Neymar, ambaye ni raia wa Brazil na miongoni mwa wachezaji mashuhuri zaidi duniani, alikabiliana na changamoto kubwa baada ya kuamua kucheza mechi tatu akiwa na jeraha hilo.
Katika mechi hizo, nyota huyo alionyesha kiwango cha hali ya juu, akifunga mabao manne na kutoa pasi moja ya bao, akithibitisha mchango wake mkubwa ndani ya Santos FC, na kuhakikisha timu hiyo inabaki Ligi Kuu.
Matokeo hayo yalimuweka Neymar kwenye kipaumbele cha mashabiki na wanahabari wa soka, huku akionyesha uthubutu wa hali ya juu licha ya maumivu yaliyokuwa yanamkabili.
Upasuaji huo utafanywa na daktari mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Rodrigo Lasmar, huku Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) likifuatilia kwa karibu kila hatua ya mchakato wa matibabu ya mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kupita Barcelona ya Hispania na Al Ahly ya Saudi Arabia.
Lengo kuu la upasuaji huo ni kumrudisha Neymar katika hali bora ya kimwili, na kuhakikisha anaendelea kuwa nyota wa timu ya taifa na kikosi cha klabu yake.
Wataalamu wa matibabu wanasisitiza kwamba, ikiwa upasuaji utafanyika kwa mafanikio na Neymar akaendelea kuwa katika kiwango chake, kuna uwezekano mkubwa akaitwa katika kikosi cha Brazil kitakachoshiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Licha ya jeraha hilo, Neymar amedhihirisha mara kadhaa kuwa msimu huu, anataka kuhakikisha anaendeleza rekodi na historia yake ya mashujaa wa Brazil, huku akionyesha mfano wa uthubutu na kujituma kwa wachezaji wadogo wanaomtazama kama mfano cha kuigwa.