Newcastle yakubali yaishe kwa Isak, mbadala wake watajwa
Muktasari:
- Larsen ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Wolves na msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote na kufunga mabao 14.
NEWCASTLE United imeonyesha nia kubwa ya kumsajili mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Norway mwenye umri wa miaka 25, Jorgen Strand Larsen katika dirisha hili la majira ya kiangazi ili akawe mbadala wa staa wao wa kimataifa wa Sweden, Alexander Isak, 25, ambaye amewaambia kuwa anataka kuondoka katika dirisha hili.
Larsen ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Wolves na msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Newcastle imevutiwa sana na Larsen kwa sababu mbali ya uwezo wake wa kufunga pia amekuwa akisaidia kutoa pasi za mwisho na msimu uliopita alitoa tano.
Mbali ya Larsen, Newcastle pia inamnyatia mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, ambaye anahusishwa pia na timu mbalimbali barani Ulaya.
Hata hivyo, inaeleweka kuwa klabu hiyo kutoka Kaskazini Mashariki mwa England inaweza kuwasajili wote ili kuziba pengo la Isak.
Ripoti zinaeleza klabu hiyo ya Ligi Kuu England inavutiwa na mchezaji huyo wa Norway ambaye timu yake inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 30 milioni ili kumuuza.
Mabosi wa Newcastle wapo tayari kumuuza Isak lakini kwa kiasi cha Pauni 130 milioni ambacho kitavunja rekodi ya ada ya uhamisho nchini England
Callum Wilson
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Newcastle United, Callum Wilson, 33, amefikia makubaliano binafsi na West Ham United ambayo atajiunga nayo kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Newcastle kumalizika mwisho wa msimu uliopita. Katika msimu uliopita staa huyo wa kimataifa wa England alicheza mechi 22 za michuano yote na awali alionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kutimkia Italia, lakini ameamua kusalia Ligi Kuu England kutokana na ofa ambayo West Ham United imempa.
Tino Livramento
MANCHESTER City imefanya mazungumzo mapya na beki wa pembeni wa Newcastle United, Tino Livramento na iko tayari kulipa zaidi ya Pauni 50 milioni kwa ajili ua mchezaji huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 22. Livramento mwenyewe anatamani kujiunga na wababe hao, lakini hataki kulazimisha usajili kwa namna yoyote badala yake atasubiri hadi timu hizo mbili zitakapofikia mwafaka juu ya masuala ya ada ya uhamisho.
Luis Diaz
BAYERN Munich imeanza tena mazungumzo na Liverpool kuhusu dili la kumsajili winga Luis Diaz, katika dirisha hili, lakini bado haijawasilisha ofa ya kutaka kumsajili. Diaz mwenye umri wa miaka 28, ni miongoni mwa wachezaji ambao wameomnba wenyewe kuondoka Liverpool katika dirisha hili ili kupata changamoto mpya sehemu nyingine. Bayern imehamia kwa fundi huyu baada ya kuona uwezekano wa kuwapata Rodrygo ni mdogo. Mkataba wa Diaz unatarajiwa kumalizika 2028.
Antony
TIMU mbili kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu Saudi Arabia zinaonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Manchester United ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Real Betis, Antony, 25. Awali, Betis ilikuwa ikipambana kuhakikisha anarudi kutokana na kiwango bora alichoonyesha, lakini inaonekana kuwa ngumu kutokana na mshahara ambao anautaka. Timu hizo za Saudia zipo tayari kumpa zaidi ya Pauni 300,000 kwa wiki kama mshahara ikiwa atakubali kujiunga katika dirisha hili.
Luke Shaw
BEKI wa kushoto wa Manchester United, Luke Shaw, mwenye umri wa miaka 30, yupo tayari kusikiliza ofa kutoka klabu za Saudi Arabia, katika dirisha hili baada ya kupewa ruhusa ya kuondoka ikiwa atahitaji kufanya hivyo. Staa huyo wa kimataifa wa England ambaye amedumu kwa misimu 11 katika kikosi cha Man United mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027.
Msimu uliopita alikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya mara kwa mara yaliyokuwa yanamwandama.
Kenan Yildiz
CHELSEA imekataliwa ofa ya zaidi ya Pauni 60 milioni na Juventus kwa ajili ya mshambuliaji wa timu hiyo na Uturuki, Kenan Yildiz, 20. Juventus inataka takriban Pauni 70 milioni ili kumuuza nyota huyo ambaye ana mkataba hadi 2029.
Ikiwa kiasi hicho kitashindikana kutoka, Juventus imesisitiza kuwa hatauzwa. Kenan alifanya vizuri katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu msimu uliopita ambapo katika mechi nne alifunga mabao matatu.
Benjamin Lecomte
FULHAM inatarajiwa kukamilisha usajili wa kwanza katika dirisha hili la majira ya kiangazi kwa kumtambulisha kipa wa Montpellier, Benjamin Lecomte, 34. Inaelezwa kwamba tayari ameshawasili England kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya kabla hajasafiri kuungana na wachezaji wenzake kwa maandalizi ya msimu ujao. Mkataba wa sasa wa Lacomte na Montpellier unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu uliopita akiwa na Montpellier alicheza mechi 30 za Ligue 1.