Ndiyo hivyo! Man United yamuweka Saka anga za Neymar, Messi Ulaya

LONDON, ENGLAND. CHEZA na Manchester United, wafunge unasafisha nyota. Hicho ndicho kilichotokea kwa winga wa Arsenal, Bukayo Saka - amebebwa na Man United na kukaa matawi ya juu kabisa na masupastaa wengine wa kutoka Ligi Kuu tano bora za Ulaya.

Saka, sasa ameungana na mastaa wa maana wa Paris Saint-Germain, Lionel Messi na Neymar kwenye anga la kibabe baada ya kufunga bao matata dhidi ya Man United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Emirates, Jumapili iliyopita. Arsenal ilishinda 3-2 katika mechi hiyo.

Mechi hiyo ya Man United, imemfanya Saka kuingia kwenye orodha ya wachezaji wanne tu wa kutoka Ligi Kuu tano bora za Ulaya waliofunga walau kuanzia mabao saba na kuasisti idadi kama hiyo ya mabao katika mechi walizotumikia timu zao kwa msimu huu.

Saka, 21, alifunga kwa shuti lake - bao lililokuwa la pili kwa Arsenal katika mechi hiyo na kuwazimisha Man United 3-2, huku miamba hiyo ya Old Trafford ikimbeba winga huyo Mwingereza na kumweka kwenye matawi ya juu ya kina Messi na Neymar kwa rekodi zao za msimu huu.

Saka alimtambuka Christian Eriksen kabla ya kufumua shuti kutoka umbali wa yadi 25 na mpira kupita chini kabis aya goli na kumshinda kipa David De Gea.

Bao hilo lilimfanya kuwafikia pia magwiji wa Arsenal, Thierry Henry na Freddie Ljungberg kwa maana ya kufunga katika mechi tatu mfululizo dhidi ya Man United. Lakini, kitu muhimu zaidi kwa Arsenal, mechi hiyo iliwafanya waweke pengo la pointi tano kileleni dhidi ya Manchester City.

Kwa mujibu wa takwimu za Squawka, Saka sasa yupo paa moja na masupastaa Messi na Neymar, sambamba na mshambuliaji wa Napoli, Khvicha Kvaratskhelia kwa mavitu yao ya msimu huu. Ni mastaa hao wanne tu ambao walau wamefunga na kuasisti kuanzia mabao saba na kuendelea kwenye ligi zao.
Kvaratskhelia ana takwimu zinazolingana na Saka (amefunga saba, ameasisti saba), wakati Messi amefunga mara nane na kuasisti 10, huku Neymar akiwa kinara wao, akiwa amefunga mara 11 na kuasisti mara 10.

Kwa maana hiyo, ni Messi na Neymar pekee ndiyo waliofunga na kuasisti mara nyingi kumzidi Saka kwenye ligi zao msimu huu. Habari njema kwa Saka ni kwamba sasa amefikisha idadi sawa ya asisti alizokuwa amepiga kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wote uliopita, licha ya msimu huu kucheza mechi 19 tu.

Na bado yupo nyuma kwa mabao manne kufikisha mabao yake aliyofunga katika msimu wa 2021/22.

Akizungumza baada ya mechi, Saka aliambia tovuti ya Arsenal kwamba anaamini bao hilo alilowafunga Man United ndilo bora zaidi alilowahi kusukumia nyavuni katika msiaha yake ya soka hadi kufikia sasa.

“Ni bao langu bora hakika. Sidhani kama kuna bao langu jingine lolote litaweza kushindana na hili na hata thamani ya bao lenyewe," alisema Saka.

Aliongeza: “Ninacheza nikiwa najiamini sana, nacheza nikiwa na tabasamu, nacheza kwa uhuru na wote wanaonizunguka wanacheza vizuri sana. Ni furaha kubwa kucheza kwenye hii timu. Nafurahia kila mechi, hakika.”

Akizungumzia ushindi huo muhimu, Saka alisema: “Sijui nitumie maneno gani. Tunafahamu hii mechi ni kubwa kiasi gani, historia ya klabu hizi mbili, pia ukitazama msimamo ulivyo, unaweza kuona ni ukubwa gani unajitokeza kwa kushinda mechi.

Tumefanikisha hilo, unaweza kuona namna tulivyoshangilia, ndio utafahamu ni namna gani ushindi ule ulikuwa na maana kubwa kwa kila mmoja wetu.”