Nchi nne zaomba kuandaa Kombe la Dunia Wanawake 2031
Muktasari:
- Katika uzinduzi rasmi wa zabuni hiyo jijini New York, maafisa wa Marekani wamethibitisha kuwa wanachama wenzao wa CONCACAF, yaani Mexico, Costa Rica na Jamaica, pia wataandaa baadhi ya mechi za fainali hizo.
Maafisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Marekani wamethibitisha kuwasilisha kwa pamoja zabuni ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia Wanawake 2031 na nchi za Mexico, Costa Rica na Jamaica.
Katika uzinduzi rasmi wa zabuni hiyo jijini New York, maafisa wa Marekani wamethibitisha kuwa wanachama wenzao wa CONCACAF, yaani Mexico, Costa Rica na Jamaica, pia wataandaa baadhi ya mechi za fainali hizo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Marekani, Cindy Parlow Cone, amesema: “Tunajivunia sana kuongoza zabuni hii ya Kombe la Dunia kwa Wanawake 2031, pamoja na washirika wetu wa CONCACAF kutoka Mexico, Costa Rica na Jamaica.
“Pamoja, tunayo nafasi ya kipekee kuandaa Kombe la Dunia kwa Wanawake kubwa zaidi na lenye athari kubwa zaidi katika historia.”
Zabuni hiyo ya pamoja inatarajiwa kupitishwa rasmi katika Mkutano wa FIFA utakaofanyika Vancouver mwaka 2026.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino alitangaza mwezi Aprili 2025 kuwa Marekani ilikuwa zabuni pekee kwa ajili ya mashindano ya mwaka 2031, lakini alieleza kuwa kuna uwezekano wa nchi zingine kutoka CONCACAF kujiunga, jambo ambalo sasa limethibitishwa.
Wakati huohuo, Infantino pia alitangaza kuwa Kombe la Dunia la Wanawake 2035 litafanyika Uingereza, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini.
Rais wa CONCACAF na Makamu wa Rais wa FIFA, Victor Montagliani, amepokea zabuni hiyo ya pamoja kwa kusema: “Dhamira ya Shirikisho letu kwa maendeleo ya soka la wanawake haijawahi kuwa imara zaidi, na kuandaa Kombe la Dunia la Wanawake 2031, ni njia mojawapo ya kuendeleza kasi hiyo.
“Tutakitia moyo kizazi kijacho cha wachezaji na mashabiki kote Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Karibiani.”