Nagelsmann amkingia kifua Wirtz, aishutumu Liverpool
Muktasari:
- Kiungo mchezeshaji Wirtz, alisajiliwa kwa Pauni 116 milioni kutokea Bayer Leverkusen, lakini hajafunga wala kuasisti kwenye mechi 11 alizoichezea Liverpool kwenye Ligi Kuu England.
MUNICH, UJERUMANI: KOCHA wa Ujerumani, Julian Nagelsmann amewashutumu wachezaji wa Liverpool wanapaswa kuboresha viwango vyao ili watumie vyema nafasi za mashambulizi zinazotengenezwa na kiungo wake, Florian Wirtz.
Kiungo mchezeshaji Wirtz, alisajiliwa kwa Pauni 116 milioni kutokea Bayer Leverkusen, lakini hajafunga wala kuasisti kwenye mechi 11 alizoichezea Liverpool kwenye Ligi Kuu England.
Lakini, Nagelsmann amesema tatizo lipo kwa wachezaji wenzake wa Liverpool hawapigi mipira kwenye nyavu.
Wirtz, 22, amejumuishwa kwenye kikosi cha Ujerumani cha kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Luxembourg na Slovakia.
Nagelsmann amesema: “Sote tunafahamu uwezo aliokuwa nao. Ni kitu cha kawaida kwa mchezaji wa umri kama wake kupungua kiwango katika vipindi fulani.
“Hatuwezi kumtarajia acheze kwenye kiwango cha juu kwa miaka mitatu mfululizo. Na badala yake tunahitaji kumpa sapoti ili kwenda anakostahili kufika na pengine Liverpool inaweza kumsaidia kwa kutumia nafasi anazozitengeneza.
“Hili haliwezi kuwa wazo la mtu mmoja tu, kwa sababu hatengenezi nafasi chache, shida wenzake hawapigi mashuti kwenye nyavu.”
Wirtz amekuwa na wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England msimu huu kutokana na namba zake kwamba hakuna bao wala asisti yoyote inayohusiana na jina lake. Amepiga mashuti 12 na kutengeneza nafasi za mashambulizi 16.