Mwanariadha Kiptum na Kocha wake wamefariki dunia kwa ajali

Mwanariadha anayeshiklia rekodi ya dunia kwenye mbio za marathon, Kelvin Kiptum raia wa Kenya amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea jana Jumapili, Februari 11, 2024.
Kiptum (24) alifariki pamoja na kocha wake, Gervais Hakizimana wa Rwanda, katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Kaptagat karibu na barabara ya Elgeyo Marakwet-Ravine.
Akithibitisha kifo hicho Kamanda wa Polisi wa Elgeyo Marakwet, Peter Mulinge alisema ndani ya gari hilo kulikuwamo na watu watatu ambao ni Kiptum akiwa na kocha wake ambao walifariki huku mwanadada aliyetambulika kwa jina Sharon Kosgey akinusurika.
Kamanda huyo amesema Kiptum alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Premio wakielekea Eldoret.
Mwanariadha huyo aliandika rekodi hiyo 2023 katika mbio za kilometa 42 Chicago nchini Marekan akimaliza kwa saa mbili na sekunde 35. Kiptum alitajwa kama mpinzani wa Eliud Kipchoge mmoja wa wanariadha wakongwe nchini Kenya.
Wanariadha hao wawili walikuwa wametajwa katika timu ya Kenya ya marathon kwa ajili ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris nchini Ufaransa mwaka huu.
Akitoa salamu zake kwa Kiptum, Waziri wa Michezo wa Kenya Ababu Namwamba aliandika kwenye mtandao wa X: "Inasikitisha sana!! Kenya imepoteza vito maalum. Sina la kusema."
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya na waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga, alisema nchi hiyo imepoteza "shujaa wa kweli" na inaomboleza "mtu wa ajabu... na kinara wa riadha wa Kenya".