Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamuzi CAS asema Senegal ni mabingwa halali AFCON 2025

Muktasari:

  • Hack amesema kuwa mamlaka ya mwisho uwanjani yapo kwa mwamuzi, na mara tu anapopuliza filimbi ya mwisho, matokeo hayawezi kubadilishwa kwa misingi ya matukio yaliyotokea kabla ya hapo.

Aliyekuwa mwamuzi wa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), Raymond Hack, ameibuka na kauli nzito inayoweza kubadilisha mwelekeo wa mgogoro wa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, akisisitiza kuwa Senegal bado ni mabingwa halali kwa mujibu wa sheria za mchezo.

Hack amesema kuwa mamlaka ya mwisho uwanjani yapo kwa mwamuzi, na mara tu anapopuliza filimbi ya mwisho, matokeo hayawezi kubadilishwa kwa misingi ya matukio yaliyotokea kabla ya hapo.

 “Mwamuzi ndiye mwenye mamlaka kamili uwanjani. Alipopuliza filimbi ya mwisho baada ya muda wa nyongeza, mshindi alikuwa Senegal. Hivyo, Senegal wanabaki kuwa mabingwa,” amesema Hack.

Kauli hiyo inakuja wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika tayari limetangaza kuibatilisha Senegal ubingwa na kuipa Morocco kufuatia tukio la utata lililotokea katika fainali.


CAF yabatilisha matokeo ya uwanjani

Katika uamuzi wake rasmi, CAF ilisema kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano baada ya wachezaji wake kutoka nje ya uwanja kwa muda wakipinga penalti iliyotolewa dakika za mwisho.

Kwa mujibu wa CAF, kitendo hicho kilikiuka kifungu cha 82 na kusababisha matumizi ya kifungu cha 84, kinachoruhusu timu inayojitoa au kugomea mchezo kuhesabiwa imepoteza kwa mabao 3-0.

Matokeo hayo yalibadilisha kabisa hatima ya fainali iliyochezwa Januari 18, 2026, ambapo Senegal ilishinda bao 1-0 baada ya muda wa nyongeza kufuatia penalti ya Brahim Díaz kuokolewa na bao la ushindi kufungwa na Pape Gueye.


Senegal yapinga, yaelekea CAS

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limepinga vikali uamuzi huo, likidai kuwa hauzingatii uhalisia wa kilichotokea uwanjani.

Kwa mujibu wa FSF, mwamuzi hakuwahi kusitisha mechi bali aliisimamisha kwa muda, na baadaye mchezo uliendelea hadi kumalizika rasmi.

FSF pia imeeleza kuwa utekelezaji wa kifungu cha 84 haukuwa sahihi kwani wachezaji walirejea uwanjani na kumaliza mechi kwa kufuata utaratibu.

Sasa Senegal imepanga kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ndani ya saa 48, huku ikiomba pia kusimamishwa kwa utekelezaji wa uamuzi wa CAF hadi kesi hiyo itakaposikilizwa.


Mvutano wa kisheria waongezeka

Kauli ya Hack inaongeza uzito wa hoja ya Senegal, hasa ikizingatiwa kuwa anafahamu kwa undani taratibu za CAS na sheria za michezo.

Iwapo msimamo wake utazingatiwa, kuna uwezekano mkubwa wa uamuzi wa CAF kupingwa na hata kubatilishwa, jambo ambalo linaweza kurejesha ubingwa kwa Senegal.

Hata hivyo, kwa sasa CAF imesimama na msimamo wake, huku Morocco ikitambuliwa rasmi kama mabingwa wa AFCON 2025 hadi pale uamuzi wa mwisho wa kisheria utakapopatikana.


Dunia ya soka yasubiri uamuzi wa mwisho

Mgogoro huu umeacha dunia ya soka ikigawanyika kati ya wanaotetea sheria za mashindano na wanaosisitiza heshima ya matokeo ya uwanjani.

Hatima ya ubingwa wa AFCON 2025 sasa ipo mikononi mwa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, ambao uamuzi wake utakuwa wa mwisho na wa kisheria.