Mtu mbili kuwania buti za De Bruyne Man City

Muktasari:
- Staa huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa na umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha Forest cha msimu huu kinachopambania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini si mchezaji pekee kwenye rada za Man City.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City ipo sokoni kumsaka mrithi wa kudumu wa kiungo Kevin De Bruyne na kwenye hilo mtego wao umetegwa huko Nottingham Forest wakimtaka staa wa timu hiyo, Morgan Gibbs-White, imeelezwa.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa na umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha Forest cha msimu huu kinachopambania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini si mchezaji pekee kwenye rada za Man City.
De Bruyne ataachana na Man City mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia miamba hiyo ya Etihad kwa muongo mmoja.
Kiungo wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz ni mchezaji mwingine kwenye rada hiyo, lakini Gibbs-White anatazamwa kama chaguo kubwa endapo kama mkurugenzi wa michezo mpya, Hugo Viana ataamua cha karibu zaidi.
Staa huyo wa Forest, ambaye alitua City Ground kwa ada iliyoweka rekodi kwenye klabu hiyo katika dirisha la majira ya kiangazi la 2022, amefunga mabao matano na asisti saba msimu huu.
Moja ya asisti zake ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Man City ya kocha Pep Guardiola, mwezi uliopita, wakati Callum Hudson-Odoi alipofunga bao pekee katika mechi hiyo.
Ripoti zinafichua kwamba Man City bado haijaamua kama inahitaji mchezaji anayefanana kabisa kwenye nafasi na De Bruyne kwa kumsajili kutoka nje au itaangalia waliopo ndani kwenye klabu. Bosi mpya wa michezo, Viana atakuwa na muda wa kuamua juu ya jambo hilo wakati atakapochukua mikoba rasmi ya Txiki Begiristain.
Wachezaji hao wawili, Gibbs-White na Wirtz wote mikataba yao itafika tamati 2027, lakini staa wa Kijerumani ni mdogo kwa miaka mitatu kwa Gibbs-White na ada yake inaweza kuwa kubwa.
De Bruyne bado hajaamua pia atakwenda wapi baada ya Man City na kinachoripotiwa ni kwamba Inter Miami inapiga hesabu ya kumchukua akacheze kwenye Ligi Kuu Marekani kwenye kikosi hicho sambamba na mastaa wengine kama Lionel Messi, Jordi Alba na Sergio Busquets.