Mtoko wa Man United huko Emirates huu hapa

MANCHESTER, ENGLAND. KESI ishafungwa. Mashabiki wa Manchester United wanakuna vichwa itakuwaje kwenye mechi yao ya Arsenal watakayocheza bila ya huduma ya kiungo wa kati, Casemiro - lakini kocha wao Erik ten Hag ashafahamu atatoka na mtoko gani hiyo kesho Jumapili huko Emirates.

Man United watasafiri kuwafuata vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal kesho huku ikielezwa hiyo ni mechi yenye maana kubwa kwenye mbio za ubingwa.  Ushindi kwa Man United itawafanya wapunguze pointi na kubaki tano dhidi ya vinara hao. Casemiro hatakuwapo baada ya kuonyeshwa kadi tano za njano.

Na sasa kinachoelezwa, nafasi ya Casemiro huenda ikazibwa na Mbrazili mwenzake, Fred. Na kama si Fred, basi Scott McTominay atakuwa pacha wa Christian Eriksen kwenye eneo hilo la kiungo.

David de Gea ataendelea kukaa golini na Jack Butland atakuwa benchi, huku Diogo Dalot anayesumbuliwa na majeruhi, Aaron-Bissaka ataziba nafasi yake kwenye beki ya kulia, huku Luke Shaw - ambaye amekuwa akifanya vyema kwenye beki ya kati kwa siku za karibuni, atapangwa kushoto. Lisandro Martinez anaweza kuwa pacha wa Raphael Varane kwenye beki ya kati, wakati Bruno Fernandes atakuwa kwenye Namba 10.

Marcus Rashford na Antony watacheza pembeni kwenye wingi ya kushoto na kulia, huku Alejandro Garnacho na Anthony Elanga wataanzia kwenye benchi na itatazamwa kama Jadon Sancho atakuwa tayari kucheza mechi hiyo. Anthony Martial atasimama kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati na kama hatakuwa fiti kiafya basi staa mpya Wout Weghorst atapewa nafasi ya kuanza kwenye eneo hilo, au kama Rashford ataanza kati na Garnacho acheze wingi ya kushoto.

Kuna wengine wanaodhani Ten Hag anaweza kumtumia Martinez kwenye nafasi ya Casemiro, lakini kocha huyo hana mpango wa kufanya hivyo.

Supastaa Fernandes alituma meseji hii kwa Arsenal, akiwaambia: “Kwa sasa mpango wetu ni kushinda mechi ijayo  — hesabu zitafanywa mwisho wa msimu. Na waliopo mbele yetu tunaocheza nao ni Arsenal kwao.”