Mtoano wa 16 bora Uefa umeanza kunoga
Muktasari:
- Timu 16 zilishiriki mechi za Jumanne na Jumatano usiku kuwania nafasi ya kufuzu raundi inayofuata ya mashindano hayo, zikiwemo Newcastle United, ambao ndio pekee kutoka Ligi Kuu England kushindwa kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.
BAKU, AZERBAIJAN: TIMU zilizofuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ziko hatua moja karibu zaidi kufahamu wapinzani wao wanaofuata baada ya michezo ya kwanza ya hatua ya mtoano (play-offs).
Timu 16 zilishiriki mechi za Jumanne na Jumatano usiku kuwania nafasi ya kufuzu raundi inayofuata ya mashindano hayo, zikiwemo Newcastle United, ambao ndio pekee kutoka Ligi Kuu England kushindwa kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.
Kikosi cha Eddie Howe kinatarajiwa kusonga mbele baada ya kupata ushindi mkubwa zaidi wa wiki dhidi ya QarabaG FK, wakati ilipowachapa wapinzani wao mabao 6-1 na hivyo kuweka uongozi mkubwa kabla ya mchezo wa marudiano wiki ijayo huko Tyneside.
Tayari Newcastle inafahamu ikifuzu itakutana na ama Barcelona ya Hispania au Waingereza wenzako, Chelsea.
Arsenal, Liverpool, Manchester City na Tottenham Hotspur ni klabu vingine vya Ligi Kuu England zilizomaliza katika nafasi nane za juu kwenye hatua ya ligi na tayari vimefuzu mtoano wa 16 bora. Ingawa bado ni mapema kupanga mipango kamili kabla ya michezo ya marudiano wiki ijayo, baadhi ya timu zina picha nzuri zaidi ya kinachowangoja.
Kwa mfano, Arsenal inajua itakutana na mojawapo ya Borussia Dortmund, Atalanta, Olympiacos au Bayer Leverkusen. Baada ya michezo ya kwanza, Dortmund na Leverkusen ziko kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kushinda mechi zao kwa mabao 2-0.
Liverpool na Spurs zitacheza dhidi ya washindi wa mechi kati ya Galatasaray dhidi ya Juventus na Club Brugge KV dhidi ya Atletico Madrid. Miamba ya Uturuki iliichapa Juventus mabao 5-2 kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Turin, huku Brugge na Atletico wakitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo wa kusisimua.
Man City inaweza kukutana na Real Madrid katika raundi inayofuata baada ya kuifunga SL Benfica bao 1-0 ugenini, katika mechi iliyogubikwa na madai ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinícius Júnior.
FK Bodø/Glimt na Inter Milan ni wapinzani wengine wanaowezekana, huku Bodø/Glimt ikiwa na uongozi wa jumla wa mabao 3-1 kuelekea mchezo wa marudiano nchini Italia.