Msikie Enzo Maresca ishu ya nidhamu mbovu Chelsea
Muktasari:
- Kutokana na hilo, Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amekanusha uvumi unaoendelea kusambaa kuhusu kikosi chake huku ishu ya nidhamu ikitajwa kuwa tatizo kwa wachezaji wa timu hiyo waliopambana usiku wa kuamkia leo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Benfica
JINAMIZI la kadi nyekundu limeendelea kuikabili Chelsea ambayo sasa mechi nne za karibuni wachezaji wake watatu wamekumbana na adhabu hiyo baada ya jana Joao Pedro kutolewa uwanjani kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Kutokana na hilo, Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amekanusha uvumi unaoendelea kusambaa kuhusu kikosi chake huku ishu ya nidhamu ikitajwa kuwa tatizo kwa wachezaji wa timu hiyo waliopambana usiku wa kuamkia leo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Benfica.
Maresca, ameulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo kuhusu alichowaambia wachezaji wake baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu ya tatu katika mechi nne za karibuni.
Kocha huyo amesema ni ngumu kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja lakini anaamini hakuna tatizo kwenye kikosi chake, licha ya changamoto hiyo ya kadi nyekundu kuwakabili.
"Mimi huwa napenda kuona hali ya utulivu kwenye kikosi changu, sipendi kuzungumzia mchezaji mmoja dhidi ya mwingine, tupo hapa kwa ajili ya Chelsea yenye umoja," amesema Maresca.
"Kadi nyekundu dhidi ya Newcastle na Flamengo zilikuwa kwa sababu ya matendo mabaya, lakini Robert Sanchez dhidi ya Man United haikuwa kwa sababu ya tendo baya, ilikuwa kwa sababu tu alitaka kulinda lango, Trevoh Chalobah dhidi ya Brighton pia ni kwa sababu alitaka kulinda lango letu lisipate madhara."
"Usiku wa leo (jana), kwa ile kadi ya pili ya njano, sidhani kama Joao Pedro alimgusa hata yule mchezaji mwingine, lakini namna tukio lilivyotokea ilikuwa hatari.
"Kwangu binafsi, siioni kama ni shida au tatizo la nidhamu, ni hali tu ambapo wakati mwingine inabidi uchukue uamuzi tofauti ili kuepuka changamoto hii. Wakati mwingine ni bora kuruhusu bao au nafasi ya bao kwa sababu unakuwa na wachezaji 11 dhidi ya 11."