Maresca awaka, mabosi waingia vyumbani
Muktasari:
- Baada ya mechi yao dhidi ya Brighton kumalizika na kupoteza kwa mabao 3-1, uongozi wa Chelsea, ukiongozwa na mmiliki mwenza Behdad Eghbali, ulijumuika na kocha Enzo Maresca kwenye chumba cha kubadilisha nguo kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amewaambia wachezaji wake waache kutoa zawadi kwa timu pinzani baada ya kumaliza pungufu kwa kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu England.
Baada ya mechi yao dhidi ya Brighton kumalizika na kupoteza kwa mabao 3-1, uongozi wa Chelsea, ukiongozwa na mmiliki mwenza Behdad Eghbali, ulijumuika na kocha Enzo Maresca kwenye chumba cha kubadilisha nguo kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji.
Maresca na matajiri hao walichukua takribani saa moja kuzungumza na wachezaji hali iliyosababisha hata kocha huyo kuchelewa kufika katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Eghbali, pamoja na wakurugenzi wa michezo Paul Winstanley na Laurence Stewart, na wataalamu wa masuala ya usajili Joe Shields na Sam Jewell, mbali ya kuzungumza na wachezaji, pia walizungumza pembeni na Maresca.
“Niliwaambia wachezaji wazi kwamba hatuwezi kuendelea kutoa zawadi kwa timu nyingine kila siku, kwa sababu hiki tunachokifanya sasa cha kuonyeshwa kadi nyekundu kila mechi ni sawa na kutoa zawadi. Hilo huwa ni kosa kubwa kwa sababu ukionyeshwa kadi nyekundu mechi hubadilika kabisa.”
Kocha huyo alithibitisha kwamba mabosi wa klabu hiyo walioingia katika chumba cha kubadilishia nguo walikuwa wameenda kuzungumza naye.
Chelsea ilimaliza ikiwa pungufu katika mechi yao dhidi ya Man United baada ya kipa Roberto Sanchez kuonyeshwa kadi nyekundu na mechi iliyopita dhidi ya Brighton, Trevoh Chalobah naye alitolewa.
“Tulikuwa tunadhibiti mchezo. Tulikuwa na mashuti mengi katika kipindi cha kwanza, tuliushika mchezo kwa asilimia 70, kila kitu kilikuwa sawa. Lakini ghafla baada ya kadi nyekundu, mpango wote ulibadilika kabisa.”