Maresca alazimisha Joao Pedro kucheza
Muktasari:
- Chelsea ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Brentford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Gtech Community, Jumamosi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amefichua amemwanzisha mchezaji Joao Pedro dhidi ya Brentford kwa lazima licha ya mchezaji huyo kuomba asianze katika mechi hiyo.
Chelsea ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Brentford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Gtech Community, Jumamosi iliyopita.
Pedro, 23, aliongoza safu ya ushambuliaji wa Chelsea na kucheza kwa dakika 79 kabla ya kutolewa na kuingizwa mchezaji mwenzake aliyesajiliwa na timu hiyo dirisha hili la majira ya kiangazi, Alejandro Garnacho.
Lakini, Maresca, 45, alisema baada ya mechi hiyo kwamba straika Pedro aliomba asicheze kutokana na hali yake, hakuwa fiti.
Hiyo ni baada ya mkali huyo wa kimataifa wa Brazil kuchezea timu yake ya taifa kwenye mechi zote mbili za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Chile na Bolivia. Lakini, kocha huyo Mtaliano aligomea ombi lake kwa sababu hakuwa na straika kweye kikosi chake baada ya kumtoa kwa mkopo Nicolas Jackson huko Bayern Munich na Liam Delap ni majeruhi.
Maresca aliulizwa kama alichagua kikosi chake kwenye mechi ya Brentford huku akiwaza juu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich itakayopigwa Jumatano.
Maresca alisema: "Joao Pedro kabla ya mechi aliniambia hayupo fiti kwa asilimia 100 hivyo aliomba asicheze. Hivyo, kama nilikuwa naifikiria Bayern Munich, badi Joao angebaki kwenye benchi tu.
"Joao alicheza kwa sababu akili yote ilikuwa kwenye mechi hiyo. Lakini, ni kweli, unapokuwa na mechi nyingi za kucheza, basi machaguo ni mengi.”
Pedro aliacha alama zake kwenye mechi hiyo baada ya kutengeneza bao la kusawazisha la Cole Palmer. Chelsea ilifunga bao la pili lililofungwa na Moises Caicedo, lakini Brentford ilisawazisha dakika za majeruhi, Fabio Carvalho.