Mpira kwao ni kazi tu, hawaupendi

LONDON, ENGLAND


UNAWEZA kudhani mwanasoka kusajiliwa na klabu kubwa ni ndoto tamu itakayokuwa imetimia kwa mchezaji husika hilo linapotimia  – lakini kumbe hilo si kwa watu wote.

Kuna baadhi, wao kuwa wanasoka ni kazi tu kama ilivyo kazi nyingine, kwamba wanacheza kwasababu ni sehemu ya kuingiza kipato na si kwa ajili ya kuwa na mapenzi na mchezo huo.

Unaweza kujiuliza ni wachezaji gani hao wa mpira wa miguu ambao waliochukulia mchezo huo kama kazi na si kwa mapenzi kabisa kwa maana ya kufanya kitu wanachokipenda.


Alex Song

Kiungo wa Cameroon, Alex Song hajawahi kujali kabisa kwamba uhamisho wake wa kwenda Barcelona akitokea Arsenal ungeweza kumfanya aende kusugua kwenye benchi tu. Staa huyo alichukulia uhamisho huo wa mwaka 2012 kama fursa ya kwenda kuwa milionea.

“Barcelona iliponiletea ofa, niliangalia ni kiasi gani cha pesa nitakwenda kuvuna na sikufikiria mara mbili,” alisema Song na kuongeza. “Nilifikiria mke wangu na watoto wangu watakavyoishi kwa starehe baada ya kustaafu soka. Nilikutana na mkurugenzi wa Barca na kuniambia sitacheza sana, mimi sikujali, nilichojua nakwenda kuwa milionea.”


Benoit Assou-Ekotto

Katika mahojiano yake aliyofanya mwaka 2010, staa huyo wa zamani wa Cameroon aliweka wazi kwamba amekuwa akicheza mpira kwa ajili ya kutafuta pesa tu na kwamba si mchezo anaoupenda.

“Nilipokuja England sikuwa namfahamu yoyote na hata England nilikuwa siijui. Nilikuja hapa kwa ajili ya kazi. Ni kazi tu. Siwezi kusema nauchukia mpira, lakini ukweli soka si mchezo wa mapenzi yangu,” alisema.

“Niliwahi mazoezini kwa ajili ya kwenda kutimiza wajibu wangu wa kikazi. Ninapomaliza mazoezi kama hakuna mechi, basi sina muda wa kugusa tena mpira wala kuangalia mechi. Nilipomaliza imeisha hiyo, naenda zangu kulala.”


David Bentley

Bentley alistaafu soka mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 29 baada ya kudai mpira umemkinai. Staa huyo anadai kwamba kipindi anacheza Arsenal kitu kilichokuwa kikimvutia ni kuwa karibu na wakali kama Ray Parlour, Tony Adams na baadhi ya wachezaji wachache kwa kuwa alikuwa akiwashabikia. Lakini, soka haukuwa ulimwengu wake halisi, kwamba kilichokuwa kinamfanya awe kwenye timu hiyo ni uwepo wa mastaa hao anaowashabikia na mambo yalipokuwa tofauti tu, alichoka na kuamua kuachana na mchezo huo jumla.


Gabriel Batistuta

Shabiki yeyote wa soka aliyeibukia miaka ya 1990 alishuhudia uwezo wa kufunga mabao wa straika Batigol – alikuwa mtambo wa mabao. Lakini, usichokijua ni kwamba staa huyo hakuwa na mapenzi kabisa na soka.

Katika moja ya mahojiano yake, supastaa huyo wa zamani wa Argentina alisema: “Sipendi soka, ni kazi yangu tu.”

Hata kwenye kitabu chake, hilo lilithibitishwa na mwandishi wake, Alessandro Rialti, ambaye alipohojiwa mwaka 1999 alisema Batistuta hakuwa kama wachezaji wengine, yeye hakupenda kabisa mpira. Na kwamba staa huyo alipoondoka kwenye mechi, basi usimuulize kabisa mambo ya mpira.


Mario Balotelli

Huyu unaweza usishangae kutokana na mchezaji huyo kushindwa kuwa siriazi. Mashabiki wengi wamekuwa wakiamini kwamba endapo kama Balotelli angekuwa siriazi kidogo tu kwenye soka, basi angekuwa mchezaji tishio sana duniani, lakini jambo hilo kwake alilifanya kama kazi na si kwa mapenzi.

Wachezaji wengi wamekuwa wakishangilia kwa nguvu kubwa na kufurahia wanapofunga mabao, lakini kwa Balotelli yeye alisema kwamba hiyo ni kazi yake, hivyo hana sababu ya kushangilia.

Alisema: “Sishangilii mabao yangu kwa sababu kufunga ni kazi yangu, kwani mesenja anapofikisha barua kwa mteja wake, anashangilia?” Aliwahi kusema na kuhoji supastaa huyo wa zamani wa Inter Milan, Manchester City, AC Milan na Liverpool.

Balotelli msimu uliopita alicheza katika klabu ya Sion ya Uswisi.