Mourinho, Solskjaer kinawaka Uturuki

Muktasari:
- Magwiji hao wa Ligi Kuu England, kwa sasa watakutana kuonyesha ubabe huko Istanbul. Makocha hao wawili watamenyana, wakati Mourinho na kikosi chake cha Fenerbahce kitakapokuwa na kasheshe zito la kuikabili Besiktas ya Solskjaer.
ISTANBUL, UTURUKI: MIAKA minne baada ya kila mmoja kushika njia zake tangu walipotupiana tambo za kutosha, hatimaye, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer watakutana tena Jumapili.
Magwiji hao wa Ligi Kuu England, kwa sasa watakutana kuonyesha ubabe huko Istanbul. Makocha hao wawili watamenyana, wakati Mourinho na kikosi chake cha Fenerbahce kitakapokuwa na kasheshe zito la kuikabili Besiktas ya Solskjaer.
Makocha hao wawili wote waliwahi kuinoa Manchester United kwa nyakati tofauti kabla ya kuwahi kukutana pia kama wapinzani kwenye ligi hiyo.
Mourinho alinyakua mataji matatu ya Ligi Kuu England katika zama zake mbili alizoinoa Chelsea, wakati Solskjaer alifanya kazi ya ukocha kwenye timu za Cardiff na Man United.
Mourinho alishinda Kombe la Ligi (Carabao) na Europa League kwa kipindi chake alichokuwa Old Trafford, wakati Solskjaer kwa kipindi chake alichokuwa Man United, alikaribia kushinda Europa baada ya timu hiyo kuchapwa kwa penalti na Villarreal, Mei 2021.
Makocha hao walipokutana, Solskjaer aliiongoza Man United kuichapa Spurs ya Mourinho mabao 3-1, wiki chache kabla ya kufutwa kazi na Daniel Levy. Kwenye mechi hiyo, makocha hao walipishana lugha.
Miaka minne imepita na sasa Solskjaer na Mourinho wataonyeshana kazi huko Uturuki kwenye mchezo wa ligi. Tangu alipochukua mikoba ya Giovanni van Bronckhorst, Solskjaer, 52, ameipandisha Besiktas kutoka nafasi ya saba hadi ya nne kwenye Turkish Super Lig, wakijiweka kwenye nafasi ya kufuzu kucheza mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza Europa League endapo kama watafanikiwa kuipiku timu inayoshika nafasi ya tatu, Samsunspor. Kwa upande wa Mourinho, timu yake inapambana kuwania ubingwa.