Cunha, Man United kuna kitu kinakuja

Muktasari:
- Staa huyo wa Wolves, Cunha amekuwa kivutio kwa klabu nyingi kutokana na kiwango chake cha msimu huu na Man United iliulizia uwezekano wa kunasa huduma yake.
LONDON, ENGLAND: BABA mzazi wa Matheus Cunha amezidisha uvumi wa kuhusu mwanaye kwenda kujiunga na Manchester United dirisha lijalo la majira kiangazi kutokana na kile alichokiposti kwenye mitandao ya kijamii.
Staa huyo wa Wolves, Cunha amekuwa kivutio kwa klabu nyingi kutokana na kiwango chake cha msimu huu na Man United iliulizia uwezekano wa kunasa huduma yake.
Cunha aliongoza mambo kuwa mazuri huko Moilineux na kuisaidia timu hiyo kutokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja. Staa huyo wa Kibrazili alisaini mkataba mpya Januari, lakini aliweka kipengele cha kuondoka mwishoni wa msimu kama kutakuwa na timu itakayokuwa inahitaji huduma yake.
Sasa Man United inahusishwa na mchezaji huyo huku uvumi huo ukichagizwa zaidi baada ya baba yake Cunha kuonekana kupendezwa na moja ya komenti kwenye mtandao wa kijamii.
Staa huyo wa Wolves aliposti picha akiwa na baba yake, Carmelo na wachezaji wenzake wa Wolves, Joao Gomes na Pedro Lima wakati wa sherehe ya kuzaliwa. Carmelo alishea picha hiyo Instagram na kuandika: "Tukipumzika kwenye sherehe ya kuzaliwa ya Pedrinho Gomes hapa Wolverhampton, Uingereza." Moja ya komenti zilizotolewa kwenye posti hiyo ilisomeka "Karibu United" - na Carmelo alibonyeza kitufe cha kuonyesha amependezwa na komenti hiyo.
Ripoti zinafichua kwamba Cunha alionyesha dalili zote kwamba yupo tayari na mpango wa kujiunga na Old Trafford na mchuano wa kuwania saini yake ni mkubwa kutokana na bei anayouzwa kuwa Pauni 62.5 milioni kutokana na kipengele kilichochomekwa kwenye mkataba wake. Kocha wa Man United, Ruben Amorim amemweka kuwa kipaumbele chake kwenye usajili wa dirisha lijalo.