Mourinho: Kweli? Kila uwanja anaocheza Vini Jr una shida
Muktasari:
- Real Madrid ilikuwa ugenini kukabiliana na Benfica katika mchezo wa mchujo wa kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mchezo huo ulisimamishwa kwa takribani dakika 10 baada ya Vinícius na wenzake kutoka nje ya uwanja katika kipindi cha pili kwa madai ya Mbrazili huyo kutamkiwa matamshi ya kibaguzi na mchezaji wa Benfica.
LISBON, URENO: JOSE Mourinho amesema kwamba “kuna jambo hutokea” katika kila uwanja anaocheza Vinícius Júnior, baada ya nyota huyo wa Real Madrid kudai kuwa alitukanwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi na Gianluca Prestianni, usiku wa Jumanne.
Real Madrid ilikuwa ugenini kukabiliana na Benfica katika mchezo wa mchujo wa kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mchezo huo ulisimamishwa kwa takribani dakika 10 baada ya Vinícius na wenzake kutoka nje ya uwanja katika kipindi cha pili kwa madai ya Mbrazili huyo kutamkiwa matamshi ya kibaguzi na mchezaji wa Benfica.
Vinícius Jr aliipatia Real Madrid bao la kuongoza dakika ya 50 katika mchezo huo uliochezwa Estadio da Luz, kabla ya kusherehekea kwa kucheza dansi karibu na bendera ya kona mbele ya mashabiki wa Benfica. Wakati mchezo kuendelea, winga huyo alibadilishana maneno na Prestianni, kisha akamripoti kwa mwamuzi kufuatia madai ya kauli ya kibaguzi.
Wakati hali ya sintofahamu ikitanda uwanjani, Mourinho alionekana akizungumza na wachezaji wa Real Madrid, akiwemo Vinícius na Kylian Mbappé. Kocha huyo wa Kireno alitoa maoni yake baada ya mechi katika mahojiano na Amazon Prime.
Mourinho amesema: “Ilikuwa iwe ni wakati wa kichaa wa mchezo, bao la kushangaza katika mechi nzuri. Vipaji hivi vina uwezo wa kufanya mambo mazuri kama hayo, lakini kwa bahati mbaya yeye (Vinícius) hakuridhika tu kufunga bao lile la ajabu na kumaliza mchezo hapo. Ukifunga bao la aina ile, unapaswa kusherehekea kwa heshima.”
Alipoulizwa kama anaamini Vinícius Jr aliwachochea mashabiki na wachezaji wa Benfica kupitia ushangiliaji wake, alijibu: “Ndiyo, naamini hivyo. Maneno waliyobadilishana, Prestianni na Vinícius, nataka kuwa huru. Sitaki kulizungumzia hilo.”
Mourinho pia alieleza kile alichokuwa akimwambia Vinícius wakati wa kusimama kwa mchezo: “Nilimwambia kwamba ukifunga bao kama lile, unasherehekea na kurudi katikati. Na alipokuwa akibishana kuhusu ubaguzi wa rangi nilimwambia kuwa mtu mkubwa zaidi katika historia ya klabu hii alikuwa mweusi (Eusebio). Klabu hii, jambo la mwisho kabisa kuwa nayo ni ubaguzi wa rangi. Kwa hiyo kama katika mawazo yake kulikuwa na jambo linalohusiana na hilo, basi hii ni Benfica.”
Katika kauli iliyozua mjadala, Mourinho mwenye umri wa miaka 63 alidai kuwa kuna utata unaomhusu Vinícius Jr katika “kila uwanja” anaocheza. Aliendelea: “Kuna kitu hakiko sawa kwa sababu hutokea katika kila uwanja. Kila uwanja anaocheza Vinícius, kuna jambo hutokea. Kila mara. Nasema tu kwamba kulikuwa na dakika 50 nzuri za soka, mamilioni ya watu wakitazama duniani kote, bao zuri kabisa na kisha mchezo ukaisha hapo.”
Wakati huohuo, Vinícius Jr ametoa taarifa yake kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Benfica katika mechi ya kwanza ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliposema: “Wabaguzi wa rangi ni waoga. Wanahitaji kujificha ili kuonyesha udhaifu wao. Lakini wanalindwa na wengine ambao, kinadharia, wana wajibu wa kuwaadhibu. Kilichotokea leo si jambo jipya katika maisha yangu au ya timu yangu. Nilipata kadi ya njano kwa kushangilia bao. Bado sielewi kwa nini. Kwa upande mwingine, ilikuwa ni itifaki iliyotekelezwa vibaya ambayo haikusaidia chochote. Sipendi kuonekana katika hali kama hizi, hasa baada ya ushindi mkubwa ambapo vichwa vya habari vilipaswa kuwa kuhusu Real Madrid, lakini ni lazima.”
Kwa upande wake, Prestianni pia amevunja ukimya wake kuhusu madai ya kumbagua Vinícius Jr kwa misingi ya rangi yake aliposema: “Nataka kuweka wazi kwamba kwa wakati wowote sikumtolea matusi ya kibaguzi Vinícius Jr, ambaye kwa masikitiko alielewa vibaya kile alichodhani amesikia. Sijawahi kuwa mbaguzi kwa mtu yeyote na nasikitika kwa vitisho nilivyopokea kutoka kwa wachezaji wa Real Madrid.”