Mourinho apiga kijembe cha Carrick Man United
Muktasari:
- Carrick, 44, amepewa jukumu hilo kwa muda baada ya Mashetani Wekundu kumfuta kazi Ruben Amorim mapema mwezi huu.
LISBON, URENO: JOSE Mourinho ameipiga kijembe Manchester United baada ya klabu hiyo kumteua Michael Carrick kuwa kocha wa muda.
Carrick, 44, amepewa jukumu hilo kwa muda baada ya Mashetani Wekundu kumfuta kazi Ruben Amorim mapema mwezi huu.
Uzoefu pekee wa Carrick kama kocha mkuu ulikuwa Middlesbrough, ambako alikaa chini ya miaka mitatu na kufikia play-offs za Championship katika msimu wake wa kwanza. Carrick pia aliwahi kuwa kocha msaidizi Manchester United chini ya Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer.
Baada ya kustaafu soka la ushindani mwaka 2018, kiungo huyo wa zamani aliunganishwa katika benchi la ufundi la Mourinho. Wawili hao walifanya kazi pamoja kwa miezi sita kabla Mourinho kufutwa kazi.
Licha ya uhusiano wake na Carrick, kocha wa sasa wa Benfica amekiri kushangazwa na uamuzi wa Man United kumteua. Mourinho anaamini makocha wenye uzoefu mkubwa ndio wanaopaswa kupewa ajira kubwa zaidi katika soka.
Baada ya Benfica kupoteza kwa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Juventus katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano, Mourinho mwenye umri wa miaka 62 amesema: “Kwangu mimi, ni jambo la kushangaza kuona makocha wasio na historia na wasio na kazi ya kuonyesha wanapewa nafasi ya kufundisha timu muhimu zaidi duniani, hilo ndilo linaloshangaza kweli.
"Wakati AC Milan wanapomchukua Allegri au Juventus wanapomchukua Spalletti au Roma wanapomchagua Gasperini mambo hayo hayashangazi kamwe.”
Carrick ana muda hadi Mei kuwashawishi mabosi wa Man United kwamba ndiye chaguo sahihi la muda mrefu. Mshindi huyo mara tano wa Ligi Kuu England alianza kazi yake kwa njia bora kabisa Jumamosi iliyopita wakati alipoiongoza Man United kuichapa Manchester City 2-0 uwanjani Old Trafford.
Mechi inayofuatia Carrick anakabiliwa na shughuli pevu ugenini kukutana na vinara wa ligi, Arsenal, ambao aliwahi kuwafunga kwenye awali wa kwanza alipokuwa kocha wa kipindi cha mpito baada ya Solskjaer kufutwa kazi mwaka 2021.