Mo Salah mambo safi huko Liverpool
Muktasari:
- Liverpool iliichapa Spurs 6-3 kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur na kujitanua kileleni kwa tofauti ya pointi nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England huku ikiwa na mechi moja mkononi na Mo Salah akifanya mambo yake.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA, Mohamed Salah ameweka rekodi tamu Ligi Kuu England na Liverpool baada ya kucheza kwa kiwango cha kibabe sana dhidi ya Tottenham Hotspur juzi Jumapili.
Liverpool iliichapa Spurs 6-3 kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur na kujitanua kileleni kwa tofauti ya pointi nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England huku ikiwa na mechi moja mkononi na Mo Salah akifanya mambo yake.
Katika mchezo huo, Liverpool ilitangulia kwa bao la Luis Diaz baada ya krosi safi ya Trent Alexander-Arnold. Alexis Mac Allister akafunga la pili kwa kichwa na baada ya James Maddison kuifungia moja Spurs, Salah akafanya yake kuisaidia Liverpool kuongeza bao jingine kabla ya mapumziko.
Fowadi huyo wa Misri alimtengenezea Dominik Szoboszlai kufanya ubao usomeke 3-1, ambapo jambo hilo lilimfanya afikishe asisti ya 10 kwenye Ligi Kuu England na mabao 13 kwenye Ligi Kuu England na kuwa mchezaji wa kwanza kuwa na tarakimu mbili kwenye asisti na kufunga kabla ya Krismasi.
Mo Salah kisha alifunga mabao mawili kwenye kipindi cha pili na hivyo kumfanya ashike namba nne kwenye orodha ya vinara wa mabao wa muda wote wa Liverpool, akimpiku gwiji Scot Billy Liddell, aliyeichezea Liverpool kati ya 1938 na 1961.
Liddell alifunga mabao 228 katika mechi 534 na kufanya timu hiyo ipachikwe jina la ‘Liddellpool’. Juu yake sasa kwenye orodha ya mabao, Mo Salah anazidiwa na Gordon Hodgson (241), Roger Hunt (285) na Ian Rush (346).