Mo Salah amkaribisha De Bruyne Liverpool

Muktasari:
- De Bruyne atafunga ukurasa wa miaka 10 akiwa na Manchester City mwishoni mwa msimu huu na mkataba wake utakuwa unamalizika.
LIVERPOOL, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mohamed Salah amemkaribisha kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne katika kikosi chao katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
De Bruyne atafunga ukurasa wa miaka 10 akiwa na Manchester City mwishoni mwa msimu huu na mkataba wake utakuwa unamalizika.
Kiungo huyo amekuwa mhimili mkubwa katika ushindi wa mataji sita ya Ligi Kuu England, Kombe la FA mara mbili na katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023.
Hata hivyo, miaka miwili iliyopita imekuwa migumu kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 kutokana na majeraha, hali iliyosababisha awe nje kwa muda mwingi.
Ingawa De Bruyne alikuwa tayari kubaki Etihad, viongozi wa klabu waliamua kutompa mkataba mpya.
Mchezaji huyo amehusishwa kuwa karibu na uhamisho wa kwenda Ligi Kuu Marekani, lakini Salah amemtolea utani akipendekeza ajiunge na Liverpool.
"Nataka kumpongeza kwa kazi yake,” Salah aliambia Sky Sports.
"Amefanya kazi ya kipekee Man City na alikuwa mchezaji bora kwenye ligi kwa kipindi chote. Namtakia kila la heri… na hapa tuna nafasi yake!"
Hata hivyo, Salah alikiri dili hilo haliwezi kufanikiwa kwa sababu ya falsafa za wamiliki wa Liverpool, FSG, ambao kwa kawaida huwa hawatoi mikataba kwa wachezaji waliozidi miaka 30.
"Falsafa ya klabu, najua jinsi wanavyoshughulika na wachezaji waliovuka miaka 30. Sikutegemea ningebaki. Sio jambo baya. Tuliona jinsi ilivyotokea hapo awali," aliongeza.
"Mimi binafsi ilichukua miezi sita hadi mazungumzo yawe mazuri na kuanzia Januari mambo yakaanza kuwa mazuri. Ilituchukua muda. Nafikiri klabu ilikuwa inajaribu kuona kama bado naweza kutoa mchango au la!"