Rashford aililia FC Barcelona akizidi kuikaushia Man United

Muktasari:
- Staa huyu ambaye nusu ya msimu huu amecheza kwa mkopo Aston Villa ambako ameonyesha kiwango kilichozivutia timu nyingi, hatarajiwi kurejea katika klabu yake mama ya Man United.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na England, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 27, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Aston Villa, yuko tayari kupunguza mahitaji yake ya mshahara ili kufanikisha dili la kwenda Barcelona.
Staa huyu ambaye nusu ya msimu huu amecheza kwa mkopo Aston Villa ambako ameonyesha kiwango kilichozivutia timu nyingi, hatarajiwi kurejea katika klabu yake mama ya Man United.
Awali, ilielezwa kwamba angerejea katika kikosi cha Man United baada ya kuzungumza na kocha Ruben Amorim, lakini hilo linaonekana kushindikana.
Hivi karibuni kumekuwa na ripoti kwamba staa wa Barcelona, Lamine Yamal, amekuwa akitumika kama sehemu ya kumshawishi staa huyu, naye pia ndiye aliyependekeza asajiliwe akiamini watakuwa na muunganiko mzuri huko Camp Nou.
Jakub Kiwior
BEKI wa Arsenal na timu ya taifa ya Poland, Jakub Kiwior, mwenye umri wa miaka 25, anawindwa tena na Napoli kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Licha ya kuhitaji saini yake tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Napoli inaitaka Arsenal ikubali kupunguza bei ya beki huyu. Kwa sasa, Arsenal inahitaji pauni 30 milioni mezani ili kumuuza.
Florian Wirtz
MANCHESTER City wanapanga kutoa pauni 180 milioni kwa ajili ya kusajili wachezaji wawili ambao ni winga wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Florian Wirtz, 22, na kiungo wa AC Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Tijjani Reijnders, 26, wote katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mastaa hawa wanasajiliwa kwa ajili ya kuboresha eneo la kiungo la Man City ambalo limekuwa na upungufu tangu kuanza kwa msimu huu.
Leroy Sane
WINGA wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Leroy Sane, 29, amekataa ofa ya mkataba mpya kutoka Bayern Munich na anahusishwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu England na La Liga zinazodaiwa kumwekea ofa nono kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Sane ni mmoja kati ya mastaa waliochangia kwa kiasi kikubwa ubingwa wa Bayern katika Bundesliga kwa msimu huu.
Jeremie Frimpong
BEKI wa kulia wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Uholanzi, Jeremie Frimpong, 24, ameripotiwa kukubali mkataba wa miaka mitano wa kujiunga na Liverpool katika dirisha lijalo.
Frimpong ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, amekuwa akiwindwa na vigogo wengi barani Ulaya tangu dirisha lililopita, lakini alikataa kujiunga nao.
Bryan Mbeumo
NEWCASTLE United imepanga kutumia pauni milioni 150 katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, wakiwa na mpango wa kusajili winga wa kulia, mshambuliaji na kipa kama vipaumbele. Maeneo ambayo timu inataka kuboresha ni kwa ajili ya kuhakikisha kikosi kinakuwa imara ili kushinda vizuri katika michuano ya kimataifa na ligi kwa msimu ujao. Miongoni mwa mastaa wanaowahitaji ni straika wa Brentford, Bryan Mbeumo.
Viktor Gyokeres
MSHAMBULIAJI wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, amesema hajui hatima yake kuelekea dirisha lijalo kwani hadi sasa bado hajafanya uamuzi licha ya kupokea ofa nono kutoka timu mbalimbali. Huduma ya mshambuliaji huyu inawindwa na vigogo kama Arsenal, Chelsea na Manchester United.
Caoimhin Kelleher
ASTON Villa wanataka kuingia kwenye vita dhidi ya Chelsea, Newcastle na Bournemouth kwa ajili ya kuipata saini ya kipa wa Liverpool, Caoimhin Kelleher, 26, kama mbadala wa Emiliano Martinez katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mbali na Kelleher, vigogo wa Villa pia wanainyatia huduma ya kipa wa Espanyol, Joan Garcia, 24.