Mmesikia! Rudiger ana jambo lake, aingia anga za Tottenham
Muktasari:
- Rudiger ambaye ana uzoefu mkubwa wa soka la England alioupata kwa kucheza Chelsea alitajwa kuwa ataondoka mwisho wa msimu huu, ikiwa ni mpango wa Madrid wa kujenga kikosi cha wachezaji wenye umri wa mdogo.
TOTTENHAM Hotspur inamtazama beki wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani, Antonio Rudiger (32), kama mbadala wa nahodha wa sasa wa timu hiyo, Cristian Romero (27) anayeweza kuondoka mwisho wa msimu huu kutimkia Real Madrid.
Rudiger ambaye ana uzoefu mkubwa wa soka la England alioupata kwa kucheza Chelsea alitajwa kuwa ataondoka mwisho wa msimu huu, ikiwa ni mpango wa Madrid wa kujenga kikosi cha wachezaji wenye umri wa mdogo.
Hata hivyo, mshahara mkubwa wa Rudiger unaonekana kuwa unaweza kuwa kikwazo kikubwa katika dili hilo kwani Spurs haipo tayari kutoa kiasi kinachofikia Euro 300,000 kwa wiki ambacho ndicho anapata kwa sasa akiwa na Madrid.
Changamoto kubwa pia inaonekana ni rekodi ya majeraha ya mara kwa mara ya Rudiger inayosababisha muda mwingi awe nje ya uwanja.
Mkataba wa sasa wa Rudiger unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi tisa za michuano yote.
Bart Verbruggen
BAYERN Munich imeonyesha nia ya kumsajili kipa wa Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi, Bart Verbruggen, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, huenda kukawa kuna ugumu baada ya timu nyingine kuingia rasmi kwenye mbio hizo na kuonyesha ziko tayari kuipiku Bayern kwa kutoa Pauni 50 milioni inayohitaji na Brighton.
Verbruggen amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na Brighton, hali iliyozivutia timu nyingi kubwa barani Ulaya.
Brighton hawana presha ya kumuuza mchezaji huyo kutokana na mkataba mrefu alionao, hivyo wako tayari kusubiri hadi itakayokidhi matarajio yao itakapowekwa mezani.
John Stones
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya England, John Stones mwenye umri wa miaka 31, anaonekana kuwa mbioni kuondoka Etihad mwishoni mwa msimu huu mara baada ya mkataba wake kumalizika.
Bayern Munich imeonyesha nia ya kumsajili beki huyo mwenye uzoefu aliyepata mafanikio makubwa akiwa na Man City. Licha ya kiwango bora alichonacho, Stones amekwua akisumbuliwa sana na majeraha yanayomweka nje ya uwanja mara kwa mara.
Marc Cucurella
ATLETICO Madrid inafanyia kazi mpango wa kumsajili beki wa Chelsea na timu ya taifa ya Hispania, Marc Cucurella, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Cucurella, ambaye ana uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto au winga anaweza akauzwa na Chelsea ambayo kwa sasa inapambana kuweka sawa hesabu zao ili kuepuka adhabu ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Morgan Gibbs-White
ASTON Villa imeonyesha nia ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Nottingham Forest na England, Morgan Gibbs-White, lakini shida kubwa inaonekana kuwa kiasi cha Pauni 65 milioni kinachohitajika na timu yake kama ada ya uhamisho.
Gibbs-White amekuwa kama moyo Forest, kutokana na mchango wake lakini ameonekana kuhitaji kuondoka kutokana na kiwango cha timu hiyo kwa sasa inayokaribia kusogea nafasi za kushuka daraja.
Forest haina mpango wa kumuuza lakini haitomzuia ikiwa timu inayomhitaji itatoa kiasi hicho cha pesa.
Nico Schlotterbeck
BORUSSIA Dortmund inapanga kumpa mkataba mpya beki wake wa kimataifa wa Ujerumani, Nico Schlotterbeck, 26, ili kuzuia jaribio la Real Madrid inayohitaji kumsajili.
Schlotterbeck ameendelea kuonyesha uimara mkubwa katika safu ya ulinzi ya Dortmund na timu hiyo inaona ikimpa mkataba mpya itaweza kumuuza kwa bei ghali zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo ana mkataba unaotarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Tangu kuanza kwa msimu huu akiwa na wababe hao kutoka Signal Iduna Park, Schlotterbeck amecheza mechi 26 za michuano yote.
Iliman Ndiaye
MANCHESTER United ipo katika nafasi ya mbele katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Everton na timu ya taifa ya Senegal, Iliman Ndiaye, 25, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Ndiaye amekuwa katika rada za vigogo wa Ulaya kwa muda sasa lakini Everton imekuwa ikifanikiwa kuzima majaribio yote ya kutaka kumsajili.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote.
Sandro Tonali
NEWCASTLE United inatarajia kumsajili kiungo wa Roma na timu ya taifa ya Italia, Lorenzo Pellegrini, 29, baada ya kuona uwezekano wa Sandro Tonali, 25, kubakia katika dirisha lijalo ni mgumu.
Hata hivyo, haitofanya usajili rasmi wa fundi huyo hadi ihakikishe kuwa imemuuza Tonali ambaye katika dirisha lililopita la majira ya baridi alitajwa kuwa angejiunga na Arsenal.
Tonali aligoma kuondoka Janari na aliwaambia wawakilishi wake kwamba atabaki hadi mwisho wa msimu ili kuona ikiwa Newcastle itafuzu Ligi ya Mabingwa au laa, kisha ndio atafanya uamuzi wa kuondoka au kubaki.