Bayern yajiondoa kwa Alvarez, Arsenal kicheko
Muktasari:
- Uamuzi huo umeongeza matumaini zaidi kwa Arsenal kuingia kwa nguvu katika mbio za kuwania saini ya mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa Ulaya.
BAYERN Munich imeripotiwa kutokuwa na mpango wa kumsajili straika wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Argentina, Julian Alvarez, 26.
Uamuzi huo umeongeza matumaini zaidi kwa Arsenal kuingia kwa nguvu katika mbio za kuwania saini ya mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa Ulaya.
Licha ya kumsajili Viktor Gyokeres katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Arsenal inatafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga zaidi, na Alvarez anaonekana kufaa mfumo wa kocha Mikel Arteta.
Mkataba wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika 2030 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao 11.
Mabosi wa Bayern walihusishwa kutaka kumsajili ili akawe mbadala wa Harry Kane ambaye haonekani kuna na muda mrefu kuendelea kucheza katika kikosi hicho kutokana na umri wake. Hata hivyo, wamesitisha kila kitu kwa sasa na wanasubiri kuona mwisho wa msimu wakifanya tathmini kwa sababu bado pia wana Nicholas Jackson ambaye hawajafanya uamuzi wa kumpa mkataba wa moja kwa moja.
Cristiano Ronaldo
NYOTA wa Al-Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, anatarajiwa kurejea uwanjani Jumamosi wiki hii baada ya kusitisha mgomo.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, amekosa mechi mbili zilizopita kutokana na kugoma kucheza kwa kile kinachoelezwa kwamba hafurahishwi na namna ambavyo klabu hiyo inaendeshwa.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote zimeanza kusuluhisha tofauti jambo linalofungua njia kurejea na kuitumikia Al-Nassr.
Marcus Rashford
HATMA ya mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 28,ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Barcelona inategemea na matokeo ya uchaguzi wa urais wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Barcelona ina mpango wa kumsajili Rashford kwa Pauni 26 milioni kutoka Manchester United, na dili hilo linatajwa kuwa sehemu muhimu ya kampeni ya urais.
Elliot Anderson
MANCHESTER City inaripotiwa kujiandaa kuwasilisha ofa ya Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Elliot Anderson, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Anderson amekuwa katika kiwango bora msimu huu, hali iliyomvutia kocha Pep Guardiola anayehitaji kuendelea kuimarisha safu yake ya kiungo. Nottingham Forest haipo tayari kumuuza.
Iliman Ndiaye
MANCHESTER United inatajwa kuwa imepanga kuelekeza macho kwa mshambuliaji wa Everton na timu ya taifa ya Senegal, Iliman Ndiaye, 25, ikiwa Marcus Rashford atahamia Barcelona kwa mkataba wa moja kwa moja.
Mabosi wa Man United wanamuona nyota huyo kama mbadala sahihi wa Rashford, lakini Everton inadaiwa kutokuwa tayari kumwachia kirahisi na huenda ikahitajika ofa nono zaidi ili kushawishi kumwachia.
Sandro Tonali
MAN United imeendelea kuongeza majina ya viungo inaotaka kuwasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi na Sandro Tonali wa Newcastle United ni miongoni mwa majina yaliyoingizwa hivi karibuni.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Italia , 25, anatajwa kuwa na thamani ya Pauni 100 milioni, dau linaloweza kuwa kikwazo kikubwa kwa Man United. Mbali ya Man United, Tonali anawindwa na Arsenal, Man City na Juventus.
Samuel Chukwueze
AC MILAN inaamini Fulham itatumia kipengele cha kutoa Pauni 21 milioni ili kumsajili mazima winga raia wa Nigeria, Samuel Chukwueze, 26.
Chukwueze kwa sasa yupo kwa mkopo katika timu hiyo ya Ligi Kuu England na amekuwa akionyesha kiwango kinachoridhisha tangu atue.
Milan inaona uwezekano wa dili hilo kukamilika kuwa mkubwa, na inahitaji sana hilo litokee.
Eli Junior Kroupi
BOURNEMOUTH inapanga kumpa mkataba mpya wenye maslahi makubwa mshambuliaji kutoka Ufaransa, Eli Junior Kroupi, 19.
Mabosi wa Bournemouth wanataka kufanya hivyo kwa ajili ya kuzima tetesi za vigogo Ulaya ikiwemo Chelsea, Liverpool, Real Madrid na Paris St-Germain ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu. Bournemouth inaamini mkataba mpya utamsaidia kubaki na kukua ndani ya kikosi.