Mlemavu kushiriki mita 400 Olimpiki

JOHANNESBURG, Afrika Kusini MWANARIADHA mwenye ulemavu raia wa hapa, Oscar Pistorius ameruhusiwa kushiriki michezo ya Olimpiki ya London. Pistorius, atakuwa mwanamichezo mlemavu wa kwanza kushindana na wanamichezo wasio na ulemavu katika mbio za mita 400 kawaida na zile za kupokezana. Awali, alizuiwa kufanya hivyo, lakini akaenda mahakamani kupinga uamuzi huo. Licha ya kutofikia viwango vya kufuzu vilivyowekwa na nchi yake, Afrika Kusini, lakini kwa sasa, Pistorius yuko huru kushiriki mbio hizo. Hata hivyo, kujumuishwa kwake katika michezo hiyo na Kamati ya Olimpiki ya nchi hiyo kumeshangaza wengi. "Leo ni siku ya furaha kubwa kwangu katika maisha!" aliandika katika mtandao wa Twitter. "Nitakuwa London kwa michezo ya Olimpiki pia ile ya Walemavu! "Ninawashukuru wote kwa kunisaidia kugfanikiwa! Kwanza Mungu, familia yangu, marafiki, washindani wangu na mashabiki wangu pia! Nyote mmenifanya kama nilivyo leo!" Pistorius alijaribu kwa mwaka mzima kukata tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki . Pia, alitaka awekewe muda maalum wa kushiriki mbio za mita 400, kitu ambacho kilipingwa na Kamati ya Olimpiki ya Afrika Kusini kwamba ni kinyume cha sheria za nchi hiyo. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kamati ya Olimpiki, Tubby Reddy aliliambia Shirika la Habari la Associated Press (AP) kwamba waliomba mwanariadha huyo aruhusiwe kushiriki licha ya kutofikia muda wa kufuzu. Timu ya mbio za mita 400 ya kupokezana ( 4x400) ya Afrika Kusini itakuwa ikijaribu kutetea medali yake ya fedha iliyoitwaa kwenye ubingwa wa dunia mwaka jana. Pistorius alikimbia katika mbio hizo na kuwa mlemabu wa kwanza kutwaa medali katika michuano ya kimataifa. Ushiriki wake utaongeza ushindani kwenye michuano hiyo ambayo tayari imeshuhudia ushindani baina ya Usain Bolt-Yohan Blake, raia wa Jamaica katika mbio za mita 100 na 200.