Miguu ya Savinho na Anna katika ardhi ya kwao!
Muktasari:
- Namaanisha Savinho na Anna, daima hawasahu kule walipotokea na hata utamaduni wao licha ya hali zao za kimaisha na kiuchumi kubadilika kwa kiwango kikubwa kwa sasa.
AKIWA anacheza kama winga wa kulia pale Manchester City, bado miguu ya Savinho, 21, pamoja na mke wake, Anna Moreira, 20, inatembea juu ya ardhi iliyowakuza hadi kuanza kujitegemea mbali na nyumbani.
Namaanisha Savinho na Anna, daima hawasahu kule walipotokea na hata utamaduni wao licha ya hali zao za kimaisha na kiuchumi kubadilika kwa kiwango kikubwa kwa sasa.
Savinho ni mchezaji anayetazamiwa kuja kufanya makubwa zaidi baadaye kutokana umri bado unaruhusu na hii ndiyo sababu Man City wamempa mkataba mrefu utakaomalizika mwaka 2031.
Licha ya mwanzo mzuri kisoka, bado anakumbuka maisha ya nyumbani - kutoka kukamua ng’ombe katika shamba la babu yake huko Sao Mateus, Brazil hadi kupata nafasi Man City, hakuna kilichombadilisha.
Hivi karibuni katika ukurasa wake wa Instagram aliposti picha akiwa na mkewe Anna pamoja na mtoto wao, ni picha waliyopiga wakiwa shambani wakitazama mifungo na kueleza ndiyo maisha yao.
"Tulikulia katika maisha ya kawaida na rahisi na ni hapo ndipo familia yetu hujikuta kila wakati. Daima ni jambo jema kurudi shambani na kuhisi amani ambayo ni hapa pekee inapopatikana," alieleza Savinho.
Kwa kifupi maisha yao ni simulizi tamu na ya kuvutia inayochanganya unyenyekevu, bidii, mapenzi ya dhati na mafanikio makubwa ya soka la kisasa barani Ulaya.
Tunasema hivyo kwa sababu katika kila hatua ya safari ya Savinho amekuwa na Anna, mwanamke aliyekuwa naye tangu utotoni na ambaye amekuwa nguzo muhimu ya mafanikio yake.
Savinho alikulia katika mazingira ya kawaida sana, maisha ya shambani yalimjengea nidhamu, unyenyekevu na moyo ya kufanya kazi kwa bidii kama kijana mwenye ndoto kubwa.
Katikati mwa mazingira hayo ndipo alipoanza safari ya mapenzi na Anna ambaye alikuja kumposa alipofikisha umri wa miaka 18 na mwaka mmoja baadaye wakafunga ndoa.
Hatua hiyo ilithibitisha ukomavu wake, si tu kama mchezaji mahiri uwanjani bali pia kama mwanamume anayejua anachotaka katika maisha na kuwa tayari kukipigania.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Brazil, Anna amekuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi muhimu ya Savinho hasa upande wa soka.
Inadaiwa ni yeye aliyemsaidia Savinho kufanya uamuzi wa kujiunga na klabu ya Girona mwaka 2023, hatua iliyompa nafasi ya kung’ara Ulaya na hatimaye kufungua mlango wa kujiunga na Man City.
Ikumbukwe mnamo Julai 2024, ndipo Man City ilikamilisha usajili wa Savinho kutoka klabu ya Ufaransa, Troyes kwa ada inayoripotiwa kufikia Pauni30.8 milioni, kwa mkataba wa miaka mitano.
Dili hilo la kucheza katika Ligi Kuu England (EPL), lilikuwa hatua kubwa katika maisha ya wanandoa hao, wakilitaja kama ndoto iliyotimia baada ya safari ndefu ya kujituma kutoka mashambani.
"Nina hamasa kubwa kufanya kazi chini ya Pep Guardiola, mmoja wa makocha bora kabisa kuwahi kutokea na najua atanisaidia kuboresha kiwango changu zaidi," alisema na kuongeza.
"Nilikuwa na wakati mzuri sana nchini Hispania na sasa ninatazamia changamoto mpya ya kucheza Ligi Kuu ya England pamoja na baadhi ya wachezaji bora zaidi duniani," alieleza Savinho.
Miezi sita baada ya kusaini Man City, yaani Desemba 2024, wanandoa hao wakatangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza, habari iliyopokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wao.
Kufikia Aprili 2025, Instagram Savinho akatangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kike ambaye walimpa jina la Zaya. Katika picha, alionekana akiwa amemlaza mtoto mchanga kifuani mwake na kumkumbatia.
"Asante Mungu wangu kwa mwaka mingine wa maisha. Zawadi bora zaidi ambayo nimeweza kupata ni Zaya," alieleza Savinho, posti ambayo ilipokea pongezi kutoka mastaa kibao akiwemo Vinicius Junior.
Mara kwa mara wanandoa hawa kuposti picha mtandaoni wakionyesha matukio mbalimbali kutoka katika familia yao lakini hasa kuhusu binti yao Zaya.
Kwa upande wake Anna, yeye ni mtaalamu wa tiba ya viungo (physiotherapist) akiwa amehitimu shahada ya Sayansi na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Universidade Federal do ABC.
Kulingana na taaluma yake, amejikita katika kusaidia watu kupona majeraha na kurejea utimamu wa kiungo, kazi ambayo alianza kuifanya tangu akiwa Brazil.
Hata hivyo, bado haijajulikana iwapo bado anafanya kazi hiyo huko Uingereza anapoishi sasa, ila kikawaida kazi yake huhitaji muda mrefu wa kufanya kazi katika vituo vya afya ili kuwahudumia wagonjwa.
Licha ya kuwa mke wa mchezaji wa kimataifa tena maarufu, Anna amechagua kuishi maisha ya faragha, akilinda maisha yake binafsi na familia kwa ujumla.
Haonekana kwenye vyombo vya habari, na ukurasa wake wa Instagram umefungwa (private), hivyo wanaoweza kuona posti zake ni wale aliyoridhia yeye tu baada ya kutuma maombi (requested).
Kwa jumla, maisha ya Savinho na Anna ni ushuhuda kwamba mafanikio ya kweli hayajengwi na vipaji pekee, bali pia na mapenzi ya kweli, msaada wa karibu, maamuzi sahihi na msingi imara wa maisha ya kawaida