Michael Carrick aweka wazi hatma yake Man United
Muktasari:
- Carrick, ambaye amefikisha takribani siku 100 tangu alipochukua jukumu la kuinoa United baada ya kuondoka kwa Ruben Amorim Januari mwaka huu, amesemaanafurahia nafasi aliyopewa na anataka kuona timu ikiendelea kuboreka badala ya kujikita kwenye mustakabali wake binafsi.
LONDON, ENGLAND: Kocha wa muda wa Manchester United, Michael Carrick amesema hana presha wala hafuatilii kwa karibu mjadala wa hatima yake katika klabu hiyo, akisisitiza kwa sasa mawazo yake yote yapo kwenye kazi aliyo nayo uwanjani.
Carrick, ambaye amefikisha takribani siku 100 tangu alipochukua jukumu la kuinoa United baada ya kuondoka kwa Ruben Amorim Januari mwaka huu, amesemaanafurahia nafasi aliyopewa na anataka kuona timu ikiendelea kuboreka badala ya kujikita kwenye mustakabali wake binafsi.
Tangu achukue mikoba hiyo ya muda, Carrick ameonekana kuleta mabadiliko makubwa na ameiongoza United kupata ushindi muhimu dhidi ya wapinzani wakubwa kama Manchester City, Arsenal na hivi karibuni Chelsea FC.
Matokeo hayo yameifanya klabu hiyo kupanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England, hatua inayoifanya iwe kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Akizungumza kabla ya mechi ya nyumbani dhidi ya Brentford, Carrick alisema: “Mara nyingi nafurahia kuwa hapa. Ninafurahia nafasi niliyo nayo. Tumepata matokeo mazuri na tuko katika hali nzuri. Bado tunataka kuendelea kuboresha zaidi.”
Alipoulizwa kuhusu lini uamuzi wa mustakabali wake utafanyika, Carrick alikwepa kuweka muda maalum, akisema hana shinikizo lolote kuhusu hilo. “Kwa kweli sijui. Sifuatilii sana suala la muda wa mwisho. Nadhani mambo yatawekwa wazi yatakapokuwa tayari. Kwa sasa niko hapa kusaidia timu na klabu kupata matokeo,” ameeleza.
Kwa upande wa kikosi, Carrick alithibitisha Harry Maguire anatarajiwa kurejea baada ya kumaliza adhabu ya kadi, huku Leny Yoro akifanyiwa tathmini ya kiafya baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Chelsea. Lisandro Martínez bado yupo nje kutokana na adhabu ya kufungiwa.
Aidha, Matthijs de Ligt anaendelea na matibabu ya jeraha la mgongo, wakati Patrick Dorgu naye bado hajawa tayari kurejea uwanjani. Hata hivyo, Carrick amesemahali ya baadhi ya wachezaji inaweza kubadilika muda wowote kabla ya mchezo ujao.