Michael Carrick afunguka kuhusu Solskjaer
Muktasari:
- Man United ilimchagua Carrick mbele ya Solskjaer walipomteua kama kocha mkuu wa muda hadi mwisho wa msimu na kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 alianza kazi hiyo vizuri wikiendi iliyopita aliposhinda dabi ya Manchester.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa muda wa Manchester United, Michael Carrick amefichua Ole Gunnar Solskjaer amekuwa akimpa sapoti na kumtia moyo licha ya kumshinda katika kinyang'anyiro cha kuwania kazi ya ukocha Old Trafford.
Man United ilimchagua Carrick mbele ya Solskjaer walipomteua kama kocha mkuu wa muda hadi mwisho wa msimu na kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 alianza kazi hiyo vizuri wikiendi iliyopita aliposhinda dabi ya Manchester.
Carrick alifanya kazi kama kocha wa kikosi cha kwanza chini ya Solskjaer wakati fundi huyo alipokuwa kocha wa Man United kwa takriban miaka mitatu.
"Nilizungumza naye," amesema Carrick. "Niko karibu naye. Tumepitia mengi pamoja, hivyo amekuwa akinipa sapoti kubwa kadri anavyoweza.
"Ni mtu ninayemheshimu sana. Alitutakia kila la kheri kabla ya mechi na alikuwa na furaha baada ya kupata matokeo mazuri (dhidi ya Man City).
Alipoulizwa kama amekuwa akichukua ushauri kutoka kwa Solskjaer, Carrick ameongeza:
“Mara kwa mara tumekuwa na mazungumzo mimi na yeye. Lakini kiuhalisia mimi si mtu wa kuwasumbua watu sana kutaka ushauri wa mambo ingawa ananisapoti."
Mchezo wa pili wa Carrick ulikuwa ni dhidi ya Arsenal, jana Jumapili na kabla ya mechi alikuwa na rekodi nzuri mara zote alizokutana na timu hiyo akiwa mchezaji na baadae kocha wa muda mwaka 2021 baada ya kukabidhiwa mikoba alipofukuzwa Solskjaer.
"Michezo ya miaka mitatu au minne iliyopita imepita, ni historia,” amesema kabla ya mechi. “Hivyo ingawa uzoefu unakusaidia katika nyakati fulani, naamini huu ni mchezo tofauti kabisa."