Messi uso kwa uso na PSG

Muktasari:
- PSG iliingia uwanjani kwenye mechi yake ya mwisho ya Kundi B ikiwa kwenye hatari ya kutupwa nje baada ya kupoteza katika mechi iliyopita, lakini mabao ya Kvicha Kvaratskhelia na Achraf Hakimi yalitosha kuivusha timu hiyo na kusonga mbele.
MIAMI, MAREKANI: MABINGWA wakutandaza soka Ulaya, Paris Saint-Germain imeichapa Seattle Sounders 2-0 na kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia la Klabu, lakini wababe wengine wa Ulaya, Atletico Madrid wamesukumwa nje licha ya kushinda 1-0 dhidi ya Botafogo.
PSG iliingia uwanjani kwenye mechi yake ya mwisho ya Kundi B ikiwa kwenye hatari ya kutupwa nje baada ya kupoteza katika mechi iliyopita, lakini mabao ya Kvicha Kvaratskhelia na Achraf Hakimi yalitosha kuivusha timu hiyo na kusonga mbele.
Atletico, ilichapwa 4-0 na PSG katika mechi yao ya kwanza, ilihitaji ushindi wa tofauti wa mabao matatu kusonga mbele, lakini bao moja ililofunga kupitia kwa mtokea benchini Antoine Griezmann halikutosha kuwavusha na Botafogo ndiye waliosonga mbele
PSG haikuwa na hofu kubwa kwenye mechi dhidi ya Seattle huko kwenye Uwanja wa Lumen, licha ya kwamba Jesus Ferreira nusura awafunge baada ya makosa ya kipa Gianluigi Donnarumma. Lakini, Kvaratskhelia alifunga baada ya kazi nzuri ya Vitinha kwenye dakika ya 35 na Hakimi kuongeza jingine dakika 66, yalitosha kuivusha timu hiyo.
Atletico haikuwa kwenye kiwango bora dhidi ya Botafogo na mara kadhaa kipa Jan Oblak alilazimika kuokoa hatari nyingi. Ilifanikiwa kushinda 1-0, shukrani kwa bao la Griezmann, lakini Botafogo ndio waliosonga mbele, ambao watakwenda kukabiliana na Wabrazili wenzao Palmeiras kwenye hatua ya 16 bora baada ya kutoka 2-2 na Inter Miami ya supastaa Lionel Messi.
Miami ilikaribia kuongoza Kundi B baada ya mabao ya Tadeo Allende na Luis Suarez kuwafanya kuongoza 2-0, kabla ya Palmeiras kusawazisha kupitia kwa Paulinho na Mauricio kwenye dakika za 80 na 87. Sare hiyo ina maana, Miami inalazimika kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi, jambo linalomfanya staa Messi kukutana na PSG kwenye hatua ya 16 bora.
Hat-trick ya straika Wessam Ali haikutosha kuipa ushindi Al Ahly na hivyo kupata sare ya 4-4 dhidi ya FC Porto na timu hizo zote mbili zimetupwa nje ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu.