Messi afanya yake Hispania

MADRID, HISPANIA

BAO la Lionel Messi na asisti aliyotoa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Hispania  hapo jana, Jumamosi  dhidi ya Sevilla vimeifanya timu hiyo  kusogea hadi nafasi ya pili huku wakiachwa nyuma kwa pointi mbili  na vinara wa La Liga, Atletico Madrid.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao Barcelona imeupata umewafanya kufikisha pointi 53 huku wakiwa mbele michezo miwili zaidi ya  Atletico Madrid wenye pointi 55 kileleni.

Barcelona walipata bao la kwanza katika mchezo huo dakika ya 29 lililofungwa na winga wa Kimataifa wa Ufaransa, Ousmane Dembele akimalizia asisti ya Messi na kuifanya miamba hiyo ya soka la Hispania kwenda mapumziko ikiwa mbele.

Jana ilikuwa siku mbaya kwa beki wa Barcelona, Clement Lenglet na Youssef En-Nesyri wa Sevilla kwa nyakati tofauti mabao yao yalikataliwa  ikionekana kuwa waliotea kabla ya kufunga.

Dakika ya 85 alionyesha umwamba wake wa kupiga msumari wa pili kwa Sevilla ambao uliwapoteza nguvu za kuchomoa na kujikuta wakipoteza pointi tatu za mchezo huo wakiwa nyumbani uwanja wao wa Ramon Sanchez Pizjuan.

Bao ambalo Messi alifunga lilikuwa la 38 dhidi ya  Sevilla, ni idadi kubwa ya mabao kufunga dhidi ya timu moja. Ushindi wa mchezo huo unaifanya Barcelona kuendelea kuwa na matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo kama Atletico Madrid watateleza.