Mendes kutoka kuuza vikapu hadi wakala wa Ronaldo

DIRISHA la usajili la majira ya baridi linakaribia. Ni wakati ambao simu za mawakala mbalimbali duniani huwa bize kuhakikisha wachezaji wanaowasimamia wanakwenda mahali wanapohitaji ama wanasaini mikataba minono itakayowanufanisha.
Duniani kuna makocha wengi wakubwa na wachezaji wengi wakubwa lakini ukiwataja Cristiano Ronaldo na Jose Mourinho bila ya shaka ni miongoni mwa watu walio na sifa hizo mbili -- Mourinho ni kocha aliyeshinda kila kitu akiwa kama kocha wa timu mbalimbali na Ronaldo ni mchezaji aliyeshinda mataji takribani yote makubwa isipokuwa Kombe la Dunia.
Naam. Licha ya ukubwa wao, utajiri, umaarufu na majivuno yao, inapotokea suala la kukutana na mtu anayeitwa Jorge Mendes huwa wanaviweka kando, huwa wapole kama alivyokuwa anatulia mtukutu Zlatan Ibrahimovic mbele ya aliyekuwa wakala wake marehemu Mino Riaola.
Ukubwa wa Mendes haujaishia kwa Ronaldo na Mourinho pekee bali kupitia kampuni yake ya Gestifute inayomiliki jumla ya wachezaji 139.
Mawakala ni watu wenye nguvu kubwa sana kwenye soka la sasa, wao ndio huamua mchezaji ataenda kucheza timu gani na atalipwa kiasi gani, muda mwingine hii imewafanya wachukiwe sana na baadhi ya makocha au timu kwa sababu huwa wanawaondoa wachezaji wanaowahitaji kwenye kikosi kwa wakati husika.
Ukubwa na umaarufu wa Mendes umejengwa kwa safari ndefu sana, kwani alishawahi hadi kuwa muuza vikapu kabla ya kufikia kuwa binaadamu aliyetajirika kupitia kazi ya uwakala wa wachezaji. Leo tumekusogezea stori ya maisha yake.
MENDES NI NANI?
Alizaliwa jijini Lisbon, Ureno Januari 1966 katika familia iliyokuwa na kipato cha chini, wakati huo walikuwa wakiishi kwenye nyumba za wafanyakazi wa serikali kwa kuwa baba yake alikuwa ni mtumishi pia.
Mama yake alikuwa ni msuka kofia za majani na vikapu ambavyo Mendes alikuwa akipewa jukumu la kuviuza kwenye fukwe ya Fonte da Telha kila wikendi.
Mbali ya vikapu, bilionea huyu akiwa na umri mdogo tu, pia alikuwa akiuza nguo sokoni. Mbali ya kazi hizo zote, Mendes alikuwa akitenga muda wa kucheza mpira kwenye uwanja uliokuwa karibu na nyumbani kwao sambamba na watoto wake.
Akiwa na umri mdogo huo huo pia aliwahi kupata kazi kwenye kiwanda cha Cornetto ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa Ice Cream na yeye kazi yake hapo ilikuwa ni kushikilia vikopo ili kujaza Ice Cream hivyo alitakiwa kushikilia koni na kuhakikisha Ice Cream haianguki sakafuni. Jambo hilo linatumika kama taswira ya maisha yake ya baadaye, kwani alijitahidi sana kuhakikisha wachezaji wake wachanga hawaanguki chini.
Baada ya msoto na maisha ya kutafuta, Mendes aliondoka jijini Lisbon alipokuwa na umri wa miaka 20 na kwenda Viana do Castelo ili kuishi na kaka yake ambaye kwa wakati huo mkewe alikuwa amepoteza maisha.
Akiwa huko aliendeleza nia yake ya kutaka kuwa mchezaji mkubwa hapo baadaye kwani alijiunga na timu ya Vianense iliyokuwa inashiriki madaraja ya chini na alikuwa akicheza kama winga wa kushoto.
Maisha kwa wakati huo yalikuwa magumu sana kwa upande wake kwa sababu hata timu aliyokuwa anaichezea haikuwa inampa mshahara zaidi ya posho, hiyo ilisababisha aangalie kitu cha kufanya kitakachomuwezesha kuendesha maisha yake.
Kwanza alihama timu kutoka Vianense hadi Lanheses na akiwa kwenye timu hiyo mpya alijipa jukumu la kuitafutia matangazo ya uwanjani ambayo yaliifaidisha timu hiyo kwa kuipatia kipato zaidi na kupitia kazi hiyo Mendes alikuwa akipata mgao kwa kila tangazo ambalo alilifanikisha kupatikana kwenye timu hiyo.
Pia, alifikia uamuzi wa kufungua duka la uuzaji wa kanda za video kazi ambayo alidumu nayo kwa muda kabla hajapata wazo la kufungua baa kwenye fukwe za Viana do Castelo iliyoitwa Luz do Mar ambayo baada ya muda aliitengeneza vizuri na kuigeuza kuwa Night Club ambayo kwa kiasi kikubwa ilipata umaarufu na ikawa inawavutia watu wengi kwenye kula bata giza liingiapo.
Akiwa hapo Mendes alifanya kazi nyingi yeye mwenyewe na kuna muda alikuwa hadi Dj. Umaarufu wa baa hiyo ulifanya baadhi ua wachezaji kutoka Braga, FC Porto na Vitoria Guimaraes kuhudhuria maeneo hayo na taratibu akawa anatengeza nao urafiki hata ikafikia wakati akawa anajuana na wachezaji lakini bado wazo la kuwa wakala halikuwepo kichwani mwake.
Akiwa anaendelea na kazi hiyo ya baa, mwaka 1996, alikutana na kocha wa zamani wa Tottenham na Wolves, Nuno Espirito Santo, ambaye kwa wakati huo alikuwa ni golikipa wa timu ya Vitoria.
Nuno alikuwa na ndoto za kuja kuwa golikipa mkubwa zaidi kwenye ulimwengu wa soka na mawazo yake na ya Mendes wote yalikuwa yakifanana ingawa Mendes kwa wakati huo alikuwa na ndoto ya kuwa tajiri.
Wawili hawa walianzisha urafiki ulikomaa siku hadi siku na ilikuwa ni kipindi hiki ambacho Mendes alianza kazi ya uwakala.
ALIVYOANZA UWAKALA
Uhusiano ulijengwa, ukaendelea hadi urafiki wa muda mrefu na huo ndio ulikuwa msingi wa Mendes kuwa wakala kupitia ushawishi wa Nuno mwenyewe aliyemuomba awe wakala wake kusimamia mazungumzo yake ya kujiunga na Deportivo de La Coruna mwaka 1996.
Wakati huo Mendes hakuwa na uzoefu wowote wa kazi hiyo lakini uaminifu wa Nuno kwake ndio uliosababisha akubali kulichukua jukumu hilo zito.
Mendes alifunga safari hadi nchini Hispania kwa kutumia gari akisafiri kwa zaidi ya maili 300, kwa ajili ya kwenda kufanya mazungumzo na rais wa Deportivo, Augusto Lendoiro.
Yakawa mazungumzo ya muda mrefu hadi kufikia muafaka wa timu hiyo kukubali kumsajili Nuno na hiyo ndio ikawa kazi yake ya kwanza akiwa kama wakala wa wachezaji.
Kwenye moja ya mahojiano ambayo yalifanywa na rais wa zamani wa Deportivo, Lendoiro aliyeongoza timu hiyo hadi 2014 alimzungumzia Mendes kama ni mtu mwenye ushawishi mkubwa sana pale awapo kwenye meza ya mazungumzo.
“Jinsi anavyoelezea mambo kwa hisia na ushawishi wake huwa ni ngumu sana kukataa jambo analopendekeza.”
Dili hilo lilijenga imani kubwa kwa Nuno na Mendes na ndio maana uhamisho wake wote akiwa kama mchezaji na baadaye kama kocha, ulisimamiwa na Mreno huyu.
Baada ya kukamilisha usajili, Mendes alivutiwa sana na kutaka kuendelea kuifanya kazi ya uwakala wa wachezaji kwa mapana zaidi.
Ukaribu wake na wachezaji uliojengwa na baa aliyokuwa anaimiliki ndio aliutumia kuwashawishi awe anasimamia uhamisho wao wa kwenda sehemu mbalimbali ingawa kwa wakati huo hakuwa wakala rasmi.
Wachezaji waliofuata kuwasimamia uhamisho wao baada ya Nuno walikuwa ni Costinha, Jorge Andrade na Deco.
Akili ya Mendes kwa muda huo ilikuwa ni jinsi gani anaweza kuliteka soko la Ureno kwanza kwa kuwa wakala mkubwa nchini humo.
Bahati nzuri kwake katika kipindi hicho kulizuka ugomvi mkubwa baina ya aliyekuwa wakala maarufu nchini humo kwa wakati huo, Jose Veiga na rais wa FC Porto, Pinto da Costa.
Mendes akatumia nafasi huyo kuwa upande wa Pinto na kumshawishi kwamba angempa wachezaji ambao wangeisaidia timu yake kwa sababu wengi wa wachezaji waliokuwa na majina makubwa kwa wakati huo walikuwa chini ya Jose Veiga.
Rais huyo alikubaliana na wazo wa Mendes hata akakubali kuwachukua wachezaji waliokuwa chini yake akianza na Costinha na Deco.
SIKIA STORI YA HUYU JAMAA NA SIMU ZAKE
Unapokuwa wakala moja kati ya vitu muhimu unavyopaswa kuwa navyo karibu muda wote ni simu yako, kupitia hiyo ndio unaweza kupata ofa kutoka timu mbalimbali duniani.
Haya ndio maisha ya Mendes, moja kati ya vitu ambavyo amekuwa karibu navyo siku zote ni simu yake na anadaiwa kuwa na simu zaidi ya mbili.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anasimulia kwamba wakati wateja wa Mendes kina Jose Mourinho, Ronaldo, Pepe, Ricardo Carvalho, Angel Di Maria na Fabio Coentrao wote walipokuwa Madrid Mendes alikuwa akipiga simu zaidi ya mara 25 kwa siku.
Alipoulizwa kuwa mara zote hizo alikuwa akimpigia kwa sababu gani, Perez alicheka na kusema: “Alipiga kila siku kunieleza mambo tofauti.”
Mbali ya Perez, rais wa zamani wa Deportivo La Coruna, Augusto Cesar Lendoiro naye aliwahi kutoa ushuhuda kuhusu Mendes kwa kusema: “Mara zote nilizokuwa naye, simu yake ilikuwa inapigwa muda wote, hadi leo najiuliza au Mendes ni mtu aliyeungwa na simu au yeye ni simu iliyokuja duniani katika umbo la mwanadamu?”
Aliyewahi kuwa mtendaji mkuu wa Manchester United na Chelsea Peter Kenyon aliwahi kusimulia kwamba kuna wakati Mendes alikuwa akimpigia simu asubuhi sana kwenye saa moja au mbili asubuhi kisha alipokuwa anapokea alisikia Mendes akisema: “Nimekupigia muda huu nikujulishe kwamba nitakupigia saa tatu.’’
Kenyan anaeleza kwamba ni moja kati ya mambo yaliyokuwa yanamkera sana kwani kama alikuwa anataka ampigie saa tatu kwanini asingempigia moja kwa moja muda huo.
Moja kati ya watu wa karibu na wakala huyu ambao licha ya uhusiano wao kikazi wamekuwa pamoja muda wote, staa wa Man United Ronaldo, naye aliwahi kutoa ushuhuda kuhusu hadithi ya simu za Mendes.
Ronaldo anaeleza kwamba yeye anamiliki namba nne za simu nne tofauti za Mendes na staa huyo anaeleza kwamba mara zote anazokutana na wakala huyo amekuwa akitumia zaidi ya saa 20 kwenye simu.
Hiyo ikiwa ni mjumuisho anavyotuma meseji na kupiga, hii inatokana na wingi wa wachezaji ambao Mendes amekuwa akiwamiliki kupitia kampuni yake ya Gestifute, ambayo kiujumla ina wachezaji wanaofikia thamani ya Pauni 700 milioni wa kike kwa wa kiume.