Mechi 6 za ubingwa kwa kina Samatta

Wednesday April 21 2021
samatta pic

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu Uturuki ‘Super Ligi’, zinatarajiwa kufikia ukingoni Mei 16 hapo ndipo itafahamika kama ni Fenerbahce anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta au ni Besiktas watakaotwaa ubingwa wa msimu huu wa 2020/21.
Zikiwa zimebaki wiki tatu na siku sita, Besiktas kasi yao inaonekana kupungua baada ya kubanwa mbavu wikiendi iliyopita kwa kulazimishwa sare wakiwa nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya MKE Ankaragucu kwenye Uwanja wa Vodafone Park, Istanbul.
Achana na matokeo ya mchezo wa jana usiku, Jumapili ambao Fenerbahce walikuwa wakicheza ugenini dhidi ya Istanbul Basaksehir, hii ni michezo yao sita ijayo ambayo inaweza kuwapa ubingwa wa Super Ligi kina Samatta au wanaweza kuutema.
Kabla ya mchezo wa jana usiku, Fenerbahce walikuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 66 walizovuna kwenye michezo 33 waliyocheza sawa na Besiktas ambao wanaongoza wakiwa na pointi 70 kileleni.
Kama watapambana na kupata pointi tatu kwenye kila mchezo ambao upo mbele yao huku wakiiombea mabaya Besiktas, lolote linaweza kutokea mwisho wa msimu.


KASIMPASA
Wikiendi ijayo, Fenerbahce watakuwa nyumbani kuikaribisha Kasimpasa ambayo inapamba kuhakikisha msimu ujao inaendelea kushiriki Super Ligi. Hawapo sehemu salama kwenye msimamo, hilo linaweza kuongeza utamu wa mchezo huo.
Rekodi zinaonyesha kwenye michezo mitano iliyopita ya timu hizo mbili, Fenerbahce wameibuka na ushindi mara tano huku Kasimpasa wakishinda mara moja tu. Hiyo ina maana kwamba chama la Samatta lina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.


ALANYASPOR
Aprili 29 watakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Bahcesehir Okullari kucheza dhidi ya Alanyanspor, wakati huo wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa wa Super Ligi watakuwa wameshacheza na Rizespor.
Kwa mujibu wa ratiba, Besiktas wataanza kucheza Aprili 27 mchezo wa raundi ya 38 kabla ya siku mbili mbele kina Samatta kuwa mzigoni.
Rekodi zinaonyesha kwamba Alanyaspor ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikiisumbua Fenerbahce kwani ndani ya michezo mitano iliyopita, wameibuka na ushindi mara mbili huku wakipoteza mara moja na kutoka sare mbili hivyo kina Samatta wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kwenye mchezo huo.


Advertisement

ERZURUMSPOR
Kwenye mchezo wa raundi ya 39, wataanza Besiktas, Mei mosi kutupa karata yao kwa kucheza dhidi ya Hatayspor, siku mbili baadaye, Fenerbahce anayoichezea Samatta itashuka dimbani kucheza dhidi ya BB Erzurumspor.
Kwa mujibu wa rekodi, Fenerbahce haijawahi kupoteza dhidi ya timu hiyo ngeni kwenye daraja la juu kabisa kwenye soka la Uturuki, wamekutana mara tatu huku chama la Samatta likiibuka na ushindi mara mbili na kutoka sare moja.


ANKARAGUCU
Uwanja wa Eryaman ambao wamekuwa wakiutumia Ankaragucu umekuwa mchungu kwenye michezo ya hivi karibuni kwa Fenerbahce kwani ndani ya michezo miwili iliyopita wameshindwa kuibuka na ushindi na badala yake wamepigwa na kutoka sare.
Wakati Fenerbahce wakikiwasha dhidi ya Ankaragucu, wapinzani wao, Besiktas watakuwa na kibarua kigumu kwelikweli cha kucheza ugenini dhidi ya Galatasaray. Katika mechi hiyo kina Samatta itawabidi wawasapoti Galatasaray licha ya uhasama wa jadi uliopo baina yao kwa miaka mingi.


SIVASSPOR
Hii inaweza kuwa kama fainali kwa Fenerbahce kutokana na ubora wa Sivasspor hasa wanapokutana nao. Ukichugulia kwenye rekodi tunaweza kwenda sawa kwani licha ya ubabe wao kwenye Ligi ya Uturuki chama la Samatta limeshindwa kuibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo kwenye michezo mitatu iliyopita ya mashindano.
Mara ya mwisho kukutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Sivasspor waligawana pointi moja moja na Fenerbahce. Ukirudi michezo ya nyuma zaidi kina Samatta walikiona cha moto kwani waliishia kutandikwa kwa mabao 2-1 na 3-1.


SAYSERISPOR
Mei 16, Fenerbahce itafunga pazia la Super Ligi ugenini dhidi ya Kayserispor huku Besiktas wakikipiga na Goztepe, rekodi zinasema kwenye mechi 3 zilizopita wakiwa na Samatta wamekuwa na matokeo mazuri dhidi ya timu hiyo.

Advertisement