Mdhamini awaingiza vitani Chelsea, Arsenal
Muktasari:
- Arsenal imetambulisha udhamini na kampuni ya Deel, inayojihusisha na malipo ya mishahara na rasilimaliwatu na wataweka tangazo lao kwenye sehemu ya mikono ya jezi za Washika Bunduki ili kuwabadili “Visit Rwanda” msimu ujao.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imecheka kwa dharau kwa madai ya Arsenal imewapiga kikumbo kwenye kunasa dili la udhamini la pesa ndefu ambalo lilikaribia kutiki huko Stamford Bridge.
Arsenal imetambulisha udhamini na kampuni ya Deel, inayojihusisha na malipo ya mishahara na rasilimaliwatu na wataweka tangazo lao kwenye sehemu ya mikono ya jezi za Washika Bunduki ili kuwabadili “Visit Rwanda” msimu ujao.
Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanadai Deel walikuwa kwenye hatua za mwisho kukubaliana na Chelsea ili wakawe wadhamini wakuu wa jezi ya The Blues watakaokuwa kifuani.
Hata hivyo, Chelsea iliziipuzia taarifa hizo kwa kuwajibu mashabiki wa mahasimu wao hao wa London na hakuna kitu kama hicho kwamba wamezidiwa ujanja kwenye dili la udhamini. Dili la Visit Rwanda lililokuwa likionekana kwenye jezi za Arsenal kwenye upande wa mikononi, lilikuwa na thamani ya Pauni 10 milioni kwa mwaka.
Chelsea kwa sasa ipo sokoni kusaka mdhamini wa mbele ya jezi yao na dili hilo ni la pesa nyingi kwa kampuni kama ya Deel isingeweza kuwa na bajeti hiyo. Chelsea yenyewe kwa mdhamini anayetokea kwenye mikono ya jezi zao, kampuni ya Vietnamm FPT ina dili la mwaka mmoja lililosainiwa Oktoba. Na dili la kuhusu mdhamini mkuu wa kifuani makubaliano yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Lakini, huko kwenye mitandao ya kijamii mashabiki wa Arsenal na Chelsea wanatambiana.
Mjadala wao ni klabu gani ni kubwa. Kwa mujibu wa utafiti wa GWI, Chelsea ina mashabiki milioni 201.7 duniano kote ukilinganisha na Arsenal yenye maskani milioni 178.3. Chelsea pia ina wafuasi milioni 147 kwenye mitandao ya Instagram, Facebook, TikTok, X na YouTube, wakati Arsenal ina wafuasi milioni 116.
Mashabiki wa Chelsea wanatamba pia kwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, wakati Arsenal haijawahi kunyakua taji hilo, huku The Blues ikibeba pia ubingwa wa Kombe la Dunia la Klabu miezi michache iliyopita. Arsenal inatamba kwenye kubeba ubingwa wa ligi mara 13 na Kombe la FA mara 14, wakati Chelsea imebeba ligi mara sita na Kombe la FA mara nane.