McTominay aambiwa ni ‘mchezaji wa kawaida’
Muktasari:
- McTominay alihama kutoka Manchester United mwaka 2024 kwa Pauni 26 milioni na amekuwa mhimili wa Napoli iliyotwaa Scudetto. Akiwa na mabao 26 katika mechi 76, alishinda tuzo ya MVP na kuiongoza timu hiyo mafanikio makubwa.
NAPOLI, ITALIA: Kiungo wa kati wa Scott McTominay ameingia kwenye mjadala mkali baada ya kupuuzwa na gwiji wa Serie A, licha ya msimu wake mzuri akiwa na Napoli, huku akishinda tuzo na kuingia kwenye orodha ya Ballon d’Or.
McTominay alihama kutoka Manchester United mwaka 2024 kwa Pauni 26 milioni na amekuwa mhimili wa Napoli iliyotwaa Scudetto. Akiwa na mabao 26 katika mechi 76, alishinda tuzo ya MVP na kuiongoza timu hiyo mafanikio makubwa.
Hata hivyo, Radja Nainggolan amemshusha hadhi, akimuita “mchezaji wa kawaida” asiye na ubora wa kiufundi wa kiwango cha juu.
Akizungumza na Sky Calcio Unplugged amesema: “Simpendi. Anafunga mabao, lakini kwa jumla wa mchezo ni wa kawaida. Hana uwezo wa kucheza kati ya mistari.”
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa kutokana na mchango wa McTominay Napoli.
Nainggolan pia alidai alikuwa bora kuliko McTominay na Hakan Çalhanoğlu, lakini akamkubali Nicolò Barella kuwa bora zaidi.
“Katika ubora wangu nilikuwa bora kuliko McTominay, lakini Barella namweka juu yangu,” amesema.
Ameongeza: “Napenda Kevin De Bruyne na Luka Modrić, hao ni wa daraja la juu.”
Hata hivyo, mashabiki wa Napoli wanaendelea kumtetea McTominay, wakimpa jina la utani “McFratm” kutokana na mchango wake mkubwa.
Kwa sasa, McTominay anaendelea kubaki mmoja wa viungo bora wa mabao Ulaya, huku mjadala ukiendelea kati ya takwimu na ubora wa kiufundi.