Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbio za ubingwa EPL… Arteta amejaa hofu!

ARTETA Pict

Muktasari:

  • Kuumia kwa beki Riccardo Calafiori kuliharibu siku ambayo kwa upande mwingine ilikuwa nzuri kwa Arsenal, ilipofuzu raundi ya tano ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu walipolitwaa kombe hilo mwaka 2020.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri majeraha yanaweza kuharibu nafasi ya timu yake kutwaa mataji manne ya kihistoria msimu huu baada ya kumpoteza nyota mwingine muhimu wakati wa mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Wigan Athletic, Jumapili iliyopita.

Kuumia kwa beki Riccardo Calafiori kuliharibu siku ambayo kwa upande mwingine ilikuwa nzuri kwa Arsenal, ilipofuzu raundi ya tano ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu walipolitwaa kombe hilo mwaka 2020.

Calafiori alipata tatizo lisilojulikana wakati wa mazoezi ya kupasha misuli kabla ya mechi, huku Martin Odegaard naye akikosekana kwenye kikosi cha siku ya mechi baada ya kupata maumivu madogo katika sare ya 1-1 dhidi ya Brentford, Alhamisi iliyopita.

Ben White naye alitolewa katika kipindi cha pili baada ya kupatiwa matibabu uwanjani, lakini baadaye aliandika kwenye Instagram kuthibitisha kuwa “hana jeraha lolote” baada ya mechi.

Calafiori na Odegaard wanaungana na Kai Havertz pamoja na Mikel Merino katika chumba cha matibabu cha Arsenal na Arteta ana wasiwasi kuwa idadi inayoongezeka ya majeruhi inaweza kuathiri harakati za timu hiyo kusaka mataji manne.

Arteta amesema: “Ndiyo nina wasiwasi. Hasa kwa sababu bado tupo kwenye mashindano. Awali walikuwa washambuliaji, kisha mabeki, sasa ni viungo. Bado tunakabiliana na hali hiyo, lakini tunahitaji baadhi ya wachezaji warejee wakiwa fiti ili watupe sio tu idadi, bali pia chaguo tofauti kulingana na wapinzani tunaokutana nao.”

Licha ya majeraha hayo, Arsenal iliicharaza Wigan ya League One kwa mabao manne ndani ya dakika 30 za kwanza, kupitia Noni Madueke, Gabriel Jesus, Gabriel Martinelli na bao la kujifunga la Jack Hunt lililowafanya wenyeji waondoke mapema kwenye matumaini.

Arteta aliwapa nafasi ya kucheza nyumbani kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa wachezaji chipukizi wa miaka 16, Marli Salmon na kipa wa miaka 19, Tommy Setford, akiwatoa benchini kutokana na matatizo ya majeraha, huku Christian Norgaard akionyesha kiwango kizuri katika kuanza kikosi mara chache kama kiungo.

Arteta amesema: "Hizi ndizo mechi wanazoweza kupata uzoefu. Hicho ndicho tunachohitaji. Tuna wachezaji muhimu ambao wako nje kwa sasa na tunahitaji kuhakikisha wako katika hali nzuri, tayari kucheza na tayari kushindana."

Arsenal itakutana na Wolves katika mchezo wa Ligi Kuu England, Jumatano, bado inapambana katika mashindano yote manne na inaweza kuwa timu ya kwanza ya England kushinda mataji manne kwa msimu mmoja, lakini italazimika kupambana na ratiba ngumu ili kufanikisha hilo.

Kulikuwa pia na mabadiliko ya kushangaza kutoka kwa Arteta, aliyemwingiza kipa wa akademi kwa mechi yake ya kwanza ya nyumbani ya kikosi cha wakubwa licha ya Kepa Arrizabalaga kuwa fiti. Mfungaji Madueke amewaambia mashabiki kuwa wana haki ya kufurahia kile ambacho klabu inaweza kufanikisha kati ya sasa na mwisho wa msimu.

Winga huyo amesema: "Nadhani mashabiki wana haki kabisa ya kuwa na msisimko. Tunafanya kazi kwa bidii kujaribu kuleta msimu unaostahili kulingana na kiwango chetu kwa sasa. Hilo ndilo lengo letu kuu na nadhani ni jambo la kusisimua, lakini tunahitaji kuendelea kufanya mambo sahihi kila siku."

 

MECHI ZIJAZO ZA ARSENAL

-Februari 18 vs Wolves (ugenini)

-Februari 22 vs Tottenham (ugenini)

-Machi 1 vs Chelsea (nyumbani)

-Machi 4 vs Brighton (ugenini)

-Machi 15 vs Everton (nyumbani)