Arsenal kubadili jezi kwachukiza mashabiki
Muktasari:
- Brentford walivaa jezi yao ya nyumbani yenye mistari mekundu na meupe pamoja na kaptura na soksi nyeusi. Kwa upande wao, Arsenal walivaa jezi yao ya ugenini ya rangi ya bluu ikiwa imeunganishwa na kaptura na soksi za kijivu hafifu.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ililazimika kufanya mabadiliko makubwa ya jezi ilipocheza ugenini dhidi ya Brentford jambo lililowakasirisha baadhi ya mashabiki.
Vinara hao wa Ligi Kuu England walikabiliana na Brentford kwenye Uwanja wa Gtech Community, Alhamisi usiku.
Brentford walivaa jezi yao ya nyumbani yenye mistari mekundu na meupe pamoja na kaptura na soksi nyeusi. Kwa upande wao, Arsenal walivaa jezi yao ya ugenini ya rangi ya bluu ikiwa imeunganishwa na kaptura na soksi za kijivu hafifu.
Hata hivyo, mashabiki makini waligundua kuwa mchanganyiko huo wa jezi haukuwa wa kawaida kwa klabu hiyo ya Kaskazini mwa London wanapocheza ugenini. Mashabiki kwenye mitandao ya kijamii waliona mabadiliko hayo, huku mmoja akiandika: “Samahani, hii ni nini? Sidhani kama nimewahi kuona Arsenal wakiwa na mchanganyiko huu wa bluu/kijivu/kijivu.”
Mwingine aliyekasirika amesema: “Arsenal inapaswa kukatwa pointi 12 kwa mchanganyiko huu wa jezi, kaptura na soksi.”
Kikosi cha Mikel Arteta kwa kawaida huvaa kaptura na soksi nyeusi pamoja na jezi yao ya bluu iliyokolea. Inaelezwa kuwa sababu ya mabadiliko hayo ni mgongano wa rangi za jezi kati ya timu hizo mbili, uamuzi uliofanywa na viongozi wa Ligi Kuu England.
Mwezi uliopita, Arsenal pia walilazimika kubadili sehemu ya jezi yao walipoenda ugenini kukipiga na Nottingham Forest. Ombi kutoka kwa waandaaji wa Ligi Kuu England liliwalazimisha kufanya mabadiliko madogo katika Uwanja wa City Ground, ambapo walibadilisha soksi zao kutoka nyeusi kwenda nyeupe. Ombi hilo lililenga kuepusha changamoto kwa mashabiki wenye matatizo ya kuona rangi (color blindness), huku ikielezwa kuwa mabadiliko ya rangi ya soksi yalisaidia utofauti wa rangi kuonekana wazi zaidi.
Arsenal pia walivaa kaptura na soksi za kijivu pamoja na jezi ya bluu katika ushindi wao wa 2-0 wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Athletic Bilbao, Septemba mwaka jana. Katika kipute hicho cha usiku wa Alhamisi, Arsenal ilishindwa kurejesha uongozi wake wa pointi sita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Brentford na hivyo pengo kubaki pointi nne tu dhidi ya Manchester City, waliopo kwenye nafasi ya pili. Noni Madueke aliifungia Arsenal bao la kuongoza kabla ya Keane Lewis-Potter kusawazisha.