Mbeumo bado anapikwa huko
Muktasari:
- Mbeumo, alisajiliwa kutoka Brentford kwa ada ya Pauni 71 milioni, hakuwamo kwenye kikosi cha Man United kilichoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham uwanjani MetLife, New Jersey katika mechi ya kirafiki.
CHICAGO, ENGLAND: STAA mpya wa Manchester United, Bryan Mbeumo atalazimika kungoja kidogo kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza kwa waajiri wake hao wapya.
Mbeumo, alisajiliwa kutoka Brentford kwa ada ya Pauni 71 milioni, hakuwamo kwenye kikosi cha Man United kilichoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham uwanjani MetLife, New Jersey katika mechi ya kirafiki.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim alifichua Mbeumo bado yupo nyuma kidogo na wenzake kwenye utimamu wa mipango yake kwenye kikosi hicho na ndiyo maana hakucheza dhidi ya West Ham.
Mbeumo hatacheza pia mechi ya pili ya Man United kwenye pre-season yao huko Marekani itakapomenyana na Bournemouth kwenye Uwanja wa Soldier Field, mjini Chicago, Jumatano, huku aijifua na wenzake kujiweka fiti zaidi kabla ya msimu mpya kuanza.
Lakini, kocha Amorim ana matumaini makubwa Mbeumo atakuwa fiti kucheza mechi yao ya mwisho ya pre-season huko Marekani itakapomenyana na Everton kwenye Uwanja wa Mercedes Benz, Atlanta wikiendi ijayo.
“Bryan ameanza taratibu,” alisema Amorim.
“Hatacheza mechi ijayo. Tunatumai kuwa na Bryan kwenye mechi ya mwisho hapa Marekani. Anajifua kwa sasa, hivyo tutaona itakavyokuwa.”
Amorim alifichua pia mshambuliaji Joshua Zirkzee naye anapambana kuwa giti kwenye majeraha madogo, huku Noussair Mazraoui alikosa mechi ya West Ham kwa sababu ya kuwa na majeruhi. Itakuwa wiki tatu kwa kocha Amorim kufanya uamuzi wa kikosi chake kabla ya Man United haijaanza msimu mpya wa Ligi Kuu England kwa kumenyana na Arsenal.
Alipoulizwa kuhusu mechi hiyo, Amorim alisema: “Nadhani hatupaswi kujiandaa tu na mechi hiyo, bali tunapaswa kuwaandaa wachezaji namna ya kucheza kila mechi, kwa sababu soka la kisasa hujui nini kitatokea.
“Viungo wengi wamekuwa wakirudi chini kukaba na mabeki wanaanzisha mashambulizi. Kwa hivyo, mambo sio kama zamani. Hivyo ni vitu vidogo unavyopaswa kujiandaa navyo kwenye mechi, unapaswa kufanya hilo mazoezini.”
Kabla ya mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Arsenal, Man United itacheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Fiorentina uwanjani Old Trafford.