Mbappe vs Yamal, vita ya tiketi ya fainali Kombe la Dunia
Muktasari:
- Yamal, ambaye hakuwahi kufikia kiwango chake bora mwanzoni mwa michuano hiyo, alianza kuonyesha makali yake katika ushindi dhidi ya Ubelgiji na sasa anaamini Hispania ipo tayari kwa mtihani mgumu dhidi ya mabingwa hao wa zamani.
NYOTA chipukizi wa Hispania, Lamine Yamal baada ya kuingoza Hispania kutinga nusu fainali, amesema kikosi chao hakiingiwi na hofu kuelekea mchezo mkubwa dhidi ya Ufaransa, akisisitiza kuwa wamefika hatua hiyo kwa lengo la kucheza mechi kubwa na kutwaa ubingwa.
Yamal, ambaye hakuwahi kufikia kiwango chake bora mwanzoni mwa michuano hiyo, alianza kuonyesha makali yake katika ushindi dhidi ya Ubelgiji na sasa anaamini Hispania ipo tayari kwa mtihani mgumu dhidi ya mabingwa hao wa zamani.
“Tumefika nusu fainali kwa ajili ya kucheza mechi kama hizi na kushinda. Sasa ni wakati wa kupumzika na kujiandaa kwa mchezo dhidi ya Ufaransa, hakika hatuwahofii hata kidogo,” alisema Yamal.
Aliongeza kuwa rekodi ya hivi karibuni dhidi ya wapinzani wao inawapa morali kubwa.
“Tuliifunga Ufaransa mara mbili zilizopita tulipokutana. Hatuogopi. Kuna matokeo mawili tu; ama wao wafike fainali ya tatu mfululizo ya Kombe la Dunia au sisi tuwafunge kwa mara ya tatu mfululizo. Sijui kitakachotokea, lakini hatuogopi.”
REKODI INAYOIPA NGUVU HISPANIA
Hispania inaingia katika pambano hilo ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Ufaransa baada ya kushinda michezo miwili ya mwisho kati ya mataifa hayo makubwa ya soka.
Katika nusu fainali ya Euro 2024, Ufaransa ilianza vizuri kupitia bao la Randal Kolo Muani dakika ya tisa, lakini Hispania iligeuza matokeo kwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika nne za kipindi cha kwanza na kushinda 2-1.
Mwaka uliofuata, mataifa hayo yalikutana tena katika mchezo wa UEFA Nations League ambapo Hispania iliongoza kwa mabao 5-1, huku Yamal akifunga mara mbili. Ufaransa ilijaribu kurejea kwa nguvu mwishoni mwa mchezo, lakini Hispania ilishinda kwa mabao 5-4.
Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente, amesema mafanikio hayo ya nyuma yanawapa imani, lakini amesisitiza kuwa mchezo wa sasa utakuwa na sura tofauti, wachezaji tofauti na malengo tofauti hivyo lazima waingie wakiwa na tahadhari.
“Ni sahihi kuamini kwamba tuna uwezo wa kuifunga Ufaransa. Nafikiri nao watakuwa na wasiwasi kuhusu sisi. Sisi ndiyo timu pekee duniani iliyoweza kuwafunga mara mbili mfululizo,” alisema.
“Hata hivyo, huu ni mchezo mpya. Timu mbili kubwa zinakwenda kukutana hivyo kila kitu kimebadilika.”
Mbappe moto, Hispania ulinzi
Ingawa Hispania imekuwa ikipanda kiwango taratibu katika michuano hiyo, Ufaransa imeonekana kuwa na kasi tangu mchezo wa kwanza na imeonyesha ubora mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
Ufaransa imeshinda mechi zote sita ilizocheza, ikifunga mabao 16, mengi kuliko timu yoyote kwenye mashindano, huku ikiruhusu mabao mawili pekee.
Kwa upande wa Hispania, imepata ushindi katika mechi tano zilizopita baada ya kutoka sare ya bila mabao dhidi ya Cape Verde katika mchezo wa ufunguzi. Kikosi hicho kimefunga mabao 11 na kuruhusu bao moja tu katika michuano yote, likifungwa na Ubelgiji kwenye robo fainali.
Tofauti kubwa kati ya timu hizo imeonekana kwa nyota wao wakuu. Nahodha wa mashambulizi wa Ufaransa, Kylian Mbappe, anaongoza kwa mchango wa mabao akiwa amehusika kwenye mabao 11, huku akiwa amefunga mabao manane na kuongoza orodha ya wafungaji pamoja na Lionel Messi.
Kwa upande wa Hispania, Yamal bado hajawa kwenye kiwango chake cha juu, akiwa amefunga bao moja pekee na hajatoa pasi ya bao katika michuano hiyo.
Vita ya miamba
Hispania itaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya Ufaransa na safu bora ya ulinzi, huku Ufaransa ikitegemea makali ya Mbappe na ushambuliaji wake uliotikisa wapinzani wote.
Swali kubwa linalosubiriwa kujibiwa ni kama Hispania itaandika historia kwa kuifunga Ufaransa kwa mara ya tatu mfululizo, au kama Wafaransa watarejea kwenye fainali nyingine ya Kombe la Dunia.