Mbappe, Vini JR, Jude mtego wa Jose Mourinho
Muktasari:
- Ikiwa hilo litatokea, Real Madrid inaweza kuwa na safu ya ushambuliaji yenye nguvu zaidi duniani, ikiwa na viongozi wa timu za taifa za England, Brazil na Ufaransa wakicheza pamoja chini ya nembo moja ya klabu hiyo.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid walimaliza msimu vibaya, bila kutwaa taji lolote na wakiwa mbali na matarajio yaliyowekwa kwa kikosi kilichotarajiwa kutawala soka la Ulaya. Mashabiki wa Madrid walimaliza msimu wakiwa na maswali mengi kuhusu timu yao.
Hata hivyo, Kombe la Dunia limebadili kabisa hali hiyo ndani ya wiki chache. Wakati Madrid ilishindwa kupata mwendelezo mzuri msimu uliopita, nyota wao watatu wakubwa Jude Bellingham, Vinicius Jr, na Kylian Mbappe wamefanya vizuri wakiwa na timu zao za taifa.
Swali sasa si kama Real Madrid ina vipaji vya kutosha. Hakuna anayebisha hilo. Kinachojiulizwa ni kama kocha Jose Mourinho ataweza kuwafanya nyota hao wafanye kazi pamoja kama wanavyofanya kwenye timu zao za taifa. Ikiwa atafanikiwa, Madrid inaweza kuwa na safu ya ushambuliaji inayotisha zaidi duniani.
Mourinho alisema “kuwa na wachezaji bora ni tatizo zuri kwa kocha. Sasa kazi yangu ni kutafuta namna ya kuifanya timu ifanye kazi kama kitu kimoja, na kuepuka matatizo yaliyokuwepo misimu iliyopita.”
Kwa utani, Mourinho pia alisema anatamani wachezaji wake waondolewe mapema Kombe la Dunia ili warudi mapema kambini kuanza maandalizi ya msimu mpya. Lakini kutokana na kiwango wanachoonyesha, hilo linaonekana kuwa gumu kutokea.
Kiungo Bellingham ameendelea kuthibitisha ubora wake akiwa na England. Katika ushindi dhidi ya Panama, alifunga bao moja na kutoa pasi ya bao, na kusaidia England kumaliza kileleni mwa kundi lao.
Katika mechi tatu za hatua ya makundi, Bellingham amehusika moja kwa moja katika mabao matatu ya England akifunga mabao mawili na kutoa asisti moja na kuonyesha uongozi mkubwa licha ya umri wake mdogo.
Baada ya mechi Jude alisema “Madrid nacheza nafasi ya chini kidogo, lakini England nacheza mbele zaidi kama namba 8 au 10. Haijalishi ninacheza wapi, muhimu ni kufanya kilicho bora kwa timu.”
Upande wa Vinicius Jr amekuwa mchezaji anayeng’aa zaidi kwenye kikosi cha Brazil chini ya Carlo Ancelotti.
Katika hatua ya makundi amehusika katika mabao manne amefunga mawili na kuasisti moja. Kwa ujumla amehusika katika asilimia 71 ya mabao yote ya Brazil kwenye mashindano.
Vinicius Jr alianza kwa kufunga bao dhidi ya Morocco, akafunga bao moja na kutoa asisti dhidi ya Haiti kabla ya kufunga mabao mawili dhidi ya Scotland.
Baada ya mechi Vinicius Jr alisema
“kulikuwa na nyakati nilishindwa kuonyesha kiwango changu. Sasa nahisi nafuu, ingawa sikuwahi kuwa na shaka kuhusu uwezo wangu kabla ya Kombe la Dunia.”
Neymar pia alimpongeza akisema “Vinicius ndiye nyota wetu katika Kombe hili la Dunia. Anaamua mechi na anafanya kazi kubwa.”
Naye Kylian Mbappe ni mashine ya mabao ya Ufaransa, ameendelea kuwa tishio kubwa kwa mabeki wote.
Katika mechi tatu za hatua ya makundi amehusika moja kwa moja katika mabao sita ya Ufaransa. Akifunga mabao manne na asisti mbili katika mechi tatu za hatua ya makundi.
Mbali na kushambulia, Mbappe ameonyesha mabadiliko makubwa katika kazi ya kujilinda, jambo ambalo mashabiki wa Real Madrid walikuwa wakilitaka.
Mbappe alisema “nimekuwa nikijidai viwango vya juu kila wakati, na ninaamini bado nahitaji kuboresha uwezo wangu wa kujilinda. Hilo ni muhimu kwa timu na nitafanya kazi kuliboresha.”
Ndoto ya mashabiki wa Real Madrid imeanza kutimia kwani nyota wao watatu kwa pamoja, Bellingham, Vinicius Jr na Mbappe wamefunga jumla ya mabao kumi na kutegeneza asisti tatu katika mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Takwimu hizo zinaonyesha kwa nini England, Brazil na Ufaransa zimeingia hatua ya mtoano zikiwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Baada ya msimu usio na mafanikio, mashabiki wa Real Madrid wanaanza kurejesha matumaini. Bellingham anaongoza, Vinicius anawasumbua mabeki, na Mbappe anaamua mechi.
Changamoto kubwa sasa ni kuona kama Mourinho ataweza kuwafanya nyota hawa watatu waonyeshe kiwango hicho hicho wakiwa pamoja katika jezi ya Real Madrid.
Ikiwa hilo litatokea, Real Madrid inaweza kuwa na safu ya ushambuliaji yenye nguvu zaidi duniani, ikiwa na viongozi wa timu za taifa za England, Brazil na Ufaransa wakicheza pamoja chini ya nembo moja ya klabu hiyo.