Modric aandika rekodi mpya Croatia akifuata nyayo za Ronaldo, Messi
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya leo, imekuwa ni ya kihistoria kwa nyota huyo ambaye amefikisha michezo 200 kwa taifa hilo akishika nafasi ya nne nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Ureno, Bader Al-Mutawa wa Kuwait na Lionel Messi wa Argentina.
TORONTO, CANADA: KIUNGO na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric ameandika rekodi mpya katika kikosi hicho baada ya kufikisha mechi 200 katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Panama kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Mechi hiyo mekuwa ni ya kihistoria kwa nyota huyo ambaye amefikisha michezo 200 kwa taifa hilo akishika nafasi ya nne nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Ureno, Bader Al-Mutawa wa Kuwait na Lionel Messi wa Argentina.
Kwa wachezaji wa kiume waliocheza zaidi ya mechi 200 za timu za taifa, Ronaldo ameichezea Ureno 230 akifuatiwa na Bader Al-Mutawa wa Kuwait 202, Lionel Messi wa Argentina 201, huku pia Modric akishika nafasi ya nne baada kucheza mechi ya 200.
Modric aliyezaliwa Septemba 9, 1985, katika jijini Zadar, Croatia, katika mechi 200 alizoichezea Croatia amehusika na mabao 60 baada ya kufunga 29 na kuasisti 31.
Nyota huyo alianza mafunzo ya soka akiwa mdogo katika akademi ya GNK Dinamo Zagreb ya Croatia na 2008, akahamia Tottenham Hotspur inayoshiriki Ligi Kuu England.
Kiwango bora alichoonyesha akiwa na Tottenham Hotspur kiliwavutia mabosi wa Real Madrid waliomsajili mwaka 2012, ambapo alikuwa mmoja wa viungo bora walioshinda mataji mbalimbali ikiwemo La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya lna Kombe la Dunia la Klabu.
Pia, anakumbukwa mwaka 2018 baada ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or akiwa mchezaji bora duniani baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa Real Madrid.
Mafanikio makubwa kwa Modric katika timu ya taifa ni kuifikisha fainali ya Kombe la Dunia 2018 huko Russia kwa mara ya kwanza, ingawa ilichapwa na Ufaransa mabao 4-2, Julai 15, 2018 na kumaliza nafasi ya pili.
Katika Kombe la Dunia 2022 Qatar, Modric akaiongoza tena Croatia kuishia nusu fainali baada ya kuchapwa na mabingwa Argentina mabao 3-0, Desemba 3, 2022, japo ilishika nafasi tatu kwa kuifunga Morocco mabao 2-1, Desemba 17, 2022.