Mbappe, Pogba, Kessie, Rudiger bure Bernabeu

REAL MADRID, HISPANIA. HAKUNA pesa ya usajili na maisha lazima yaendelee. Real Madrid inatafuta namna ya kutoboa kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi na pesa ya kusajili mastaa inaowataka haipo.

Sasa miamba hiyo ya Bernabeu imepata njia mbadala ya kuhakikisha inanasa vichwa vyote vya maana kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwakani, lakini bila ya kutoa senti yoyote kwenye uhamisho. Kwa maana hiyo, inahitaji wachezaji wa bure.

Kwa muda mrefu, miamba hiyo ya LaLiga imekuwa ikifukuzia huduma ya straika wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe. Na kitu kizuri ni Mfaransa huyo atapatikana bure kabisa kwenye dirisha hilo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutokana na mkataba wake huko Parc des Princes kufika tamati mwishoni mwa msimu huu.

Mchezaji mwingine wanayemtaka ni kiungo wa Manchester United, Paul Pogba - ambaye pia mkataba wake utafika tamati mwisho wa msimu huu, atapatikana bure, huku staa mwingine ni beki wa kati wa Chelsea, Antonio Rudiger - ambaye pia atakuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu kutokana na mkataba wake huko Stamford Bridge kuelekea ukingoni na utakwisha dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Supastaa wa nne, ambaye Real Madrid inapiga hesabu kali za kunasa bure huduma yake ni kiungo wa AC Milan na Ivory Coast, Franck Kessie.

Kitu kizuri kwa Los Blancos ni itaweza kuwasainisha mikataba ya awali kwenye dirisha la Januari mastaa wote hao wanne kabla ya kutua rasmi huko Bernabeu mwishoni mwa msimu wakati usajili wa dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kitu pekee ambacho kitawapa wakati mgumu Real Madrid ni kwenye mishahara ya wakali hao, ambao wote si wachezaji wa kuhitaji kulipwa kiduchu, huku wakitambua watakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwenye timu nyingine ambazo zinahitaji pia saini za wakali hao.

Dirisha la usajili wa Januari litakuwa la vuta nikuvute kutokana na mastaa wengi mikataba yao kuelekea ukingoni, hivyo timu zitahaha kuwasainisha mikataba ya awali ili iwanase bure mwisho wa msimu kama hawatakuwa wamesaini dili mpya kwenye klabu zao wanazochezea kwa sasa.

Supastaa Mbappe alisema kwamba anafikiria kuwa mbali na PSG huku akiweka wazi dhamira yake ya kwenda kushindana kwingineko.

Pogba kwa muda mrefu amekuwa akisumbuana na Man United juu ya mkataba mpya na hawezi kuacha ipite fursa ya kwenda kukipiga Bernabeu, huku Rudiger akiwa kwenye mazungumzo ya dili jipya na The Blues, lakini hakuna kilichoafikiwa tayari baada ya mabosi wa Chelsea kugomea kumpa ofa anayotaka beki huyo wa Kijerumani, hasa kwenye mshahara.

Huko Milan, ripoti zinadichua kwamba Rossoneri yenyewe imeshakubali yaishe kwa Kessie, wamekubali aondoke na kuna timu nyingi zinahitaji saini yake ikiwamo PSG na Tottenham Hotspur inayonolewa na Antonio Conte kwa sasa.