Mbappe macho kodo kwenye Pichichi

Muktasari:
- Fowadi huyo, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa Ufaransa alifunga mara mbili dhidi ya Celta Vigo huko Bernabeu, wakati alipoifanya Los Blancos kuongoza 3-0 baada ya Arda Guler kufunga bao la kwanza.
MADRID, HISPANIA: SUPASTAA straika, Kylian Mbappe ameangusha rekodi moja baada ya nyingine kutokana na kasi yake ya kutikisa nyavu kwenye kikosi chake Real Madrid huko Hispania.
Fowadi huyo, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa Ufaransa alifunga mara mbili dhidi ya Celta Vigo huko Bernabeu, wakati alipoifanya Los Blancos kuongoza 3-0 baada ya Arda Guler kufunga bao la kwanza.
Celta ilipambana kusawazisha, lakini ilikomea kwenye mabao 3-2, huku Mbappe akiwa na sababu kibao za kufurahia siku hiyo.
Mabao yake yalikuwa ya 23 na 24 msimu huu kwenye LaLiga, akibakiza bao moja tu kumfikia kinara wa mabao, Robert Lewandowski kwenye mchakamchaka huo wa La Liga msimu huu.
Endapo atafanikiwa kumpiku Lewandowski wa Barcelona atakwenda kunyakua tuzo ya ‘Pichichi’ inayotolewa kwa kinara wa mabao kwenye La Liga, huku Mbappe atakuwa amefanya hivyo kwenye msimu wake wa kwanza kitu ambacho mashujaa wake wote walishindwa.
Supastaa Cristiano Ronaldo, aliyeondoka Madrid mwaka 2018 akiwa na tuzo tatu za Viatu vya Dhahabu vya LaLiga, hakuwa kinara wa mabao kwenye msimu wake wa kwanza Bernabeu.
Supastaa Lionel Messi aliibuka kinara wa mabao kwenye LaLiga msimu wa 2009/10, lakini hakufanya hivyo kwenye msimu wake wa kwanza kucheza kwenye La Liga. Mabao hayo yamemfanya Mbappe afikishe 36 kwenye michuano yote, ikiwani moja tu nyuma ya Ivan Zamorano, ambaye aliweka rekodi ya kufunga mara 37 katika msimu wake wa kwanza 1993.
Madrid imekuwa maarufu kwa kufanya usajili wa mastaa wenye majina makubwa Galactico, hasa kwa wale wanaocheza kwenye safu ya ushambuliaji, lakini ni wachache sana waliofanya vyema kwenye La Liga katika msimu wao wa kwanza na wakali hao ni watatu tu, Ruud van Nistelrooy, Hugo Sanchez na gwiji Alfredo Di Stefano.
Ronaldo si staa pekee mwenye jina kubwa alishindwa kufanya vizuri sana kwenye msimu wake wa kwanza katika kikosi cha Los Blancos - kutokana na kuwapo na orodha ya wakali wengine kibao akiwamo Karim Benzema, Ronaldo Nazario na Gareth Bale.
Pichichi imekuwa haina makazi ya kudumu Bernabeu tangu alipoondoka Ronaldo na tuzo hiyo ilinaswa mara moja tu tangu wakati huyo, alipofanya hivyo Benzema kwenye msimu wa 2021/22. Na sasa Mbappe anasubiriwa kama atafanikiwa kunasa tuzo hiyo.